Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Mwinyi
SERIKALI imesema itaendelea kuhakikisha wanafunzi wanaosoma nje wanakuwa katika mazingira salama, na tayari watu watano waliohusika na tukio la kushambuliwa kwa wanafunzi wanne wanaosoma India wanashikiliwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Mwinyi aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi wa tukio lililotokea Bangalore India.
“Tulipata taarifa kuwa wananchi wetu ambao ni wanafunzi wa Bangalore India walishambuliwa baada ya raia wa Sudan kumgonga raia wa India kwa gari na kisha kufariki dunia, ambapo kuanzia hapo palitokea mtafaruku wa kushambulia watu wenye asili ya Afrika waliokuwepo maeneo hayo,” alieleza Balozi Mwinyi.

Alisema baada ya tukio hilo wanafunzi hao wa Kitanzania wakitokea chuo walisimama maeneo hayo ili kujionea ni nini kimetokea lakini wao pia walichanganywa na kuanza kushambuliwa na raia hao wa India kwa kuwa walikuwa hawatofautishi watu, bali walikuwa wakishambulia raia wote wenye asili ya Kiafrika.
“Katika tukio hilo raia wetu wanne walishambuliwa vibaya na baadaye walipelekwa hospitali na kupatiwa matibabu. Kufuatia hilo balozi wetu nchini humo amefuatilia hili na ameandika barua ya kibalozi kutaka Serikali ya India kueleza ni kitu gani kimetokea na kueleza jinsi gani wanawalinda raia wetu,” alieleza.
Aidha, alisema jana Balozi wa Tanzania nchini humo amefanya ziara ya kutembelea jimbo hilo na atazungumza na raia ili kuhakikisha usalama wao unalindwa.
Pia alisema jana alimuita Balozi wa India nchini na kufanya naye mazungumzo na alimhakikisha kwamba tayari hatua zimeshachukuliwa na tamko limeshatolewa la kilichotokea Bangalore na wameahidi kwamba watahakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Alisema katika hatua za awali tayari watu watano wameshakamatwa na ulinzi wa wanafunzi umeimarishwa na kuahidi wataimarisha usalama zaidi ili wananchi walio nje waishi kwa usalama na mabaya zaidi yasijitokeze.
Aidha, Balozi Mwinyi alisema kuna tukio lingine limetokea juzi jioni la mwanafunzi Mtanzania Christian Benjamin Mutandisi aliyekuwa akisoma Chuo cha Koshys ambaye alipata ajali ya pikipiki na kufariki dunia papo hapo na kubainisha kwamba baada ya uchunguzi wamegundua kwamba ajali hiyo haihusiani na tukio la Bangalore.
“Tumegundua kwamba mwanafunzi huyo hakuvaa kofia ngumu, tumepata taarifa kwamba Jumuiya ya Watanzania inaendelea na taratibu za mazishi. Hivyo tukio hili halihusiani kabisa na lile la Bangalore,” alisema.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga alilitolea taarifa tukio hilo jana bungeni mjini Dodoma kutokana na Mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 47 uliotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).
Zitto alisema pamoja na kauli hiyo, Serikali ya India iombe radhi kwa Serikali ya Tanzania kwa kushindwa kuwalinda wanafunzi hao wanaosoma nchini mwao kwa kufuata taratibu na sheria.