Kamishna wa Maadili Jaji mstaafu Salome Kaganda
SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema kuna baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri, ambao hawajajaza fomu ya mali na ahadi ya uadilifu.
Imesema imewasilisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, orodha ya majina ya mawaziri na naibu mawaziri hao, ambao hawajawasilisha wala kujaza fomu za kutamka rasilimali, maslahi na madeni na kutosaini hati ya kiapo cha ahadi ya uadilifu.
Pia Sekretarieti hiyo imesema kutokana na uhaba wa fedha kwa muda wa miaka mitatu, haijawahi kuhakiki wala kufanya uchunguzi wa matamko ya mali za viongozi yaliyowasilishwa kwa sekretarieti hiyo.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo kwa mawaziri na naibu mawaziri kuhusu Sheria ya Maadili, Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu, Kamishna wa Maadili Jaji mstaafu Salome Kaganda, alisema hadi sasa ofisi yake imepokea fomu za matamko ya mali chache kutoka kwa mawaziri ; na wengi wao hawajajaza fomu hizo wala za ahadi ya uadilifu.
Alisema Sheria ya Maadili inamtaka kila kiongozi, kuwajibika kuwasilisha tamko la mali kwa sekretarieti hiyo.
“Nasikitika kuwa hadi sasa kuna baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri ambao hawajajaza fomu ya mali na ahadi ya uadilifu, naomba mheshimiwa Waziri Mkuu nikukabidhi orodha yao kwa hatua zaidi,” alisisitiza Jaji Kaganda.
Alisema jukumu la chombo hicho cha kusimamia maadili ya viongozi ni kupokea fomu za tamko la kiongozi wa umma za rasilimali, maslahi na madeni, kupokea kuchambua na kuchunguza malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa umma na kuandaa na kutunza daftari la rasilimali, maslahi na madeni ya viongozi hao.
Aidha alisema pia sekretarieti hiyo ina wajibu wa kuratibu vikao vya Baraza la Maadili kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kuwasilisha kwa Rais taarifa hizo za uchunguzi.
Alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 , inatamka maadili yanayotakiwa kuzingatiwa na kila kiongozi kuwa ni uadilifu, haki na uwajibikaji ambazo ni sifa muhimu za kiongozi bora.
Jaji Kaganda alisema kwa kuzingatia misingi na miongozo hiyo, katika Sheria hiyo ya maadili mawaziri na wakuu wa mikoa wanacho kifungu maalumu kinachobainisha maadili wanayopaswa kuyatekeleza.
“Tunategemea baada ya mafunzo haya mtakuwa nuru na kioo cha mfano wa uongozi kwa wananchi, hatutegemei kuona mkitunishiana misuli,” alisisitiza. Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo mawaziri watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
“Sote tumeshuhudia namna Rais John Magufuli alivyoumia namna nchi ilivyopoteza maadili. Amewaamini na kuwapa nafasi ya kumsaidia kurejesha heshima ya nchi,” alisema.
Alisema sekretarieti hiyo imepokea malalamiko hasa kutokana na Serikali iliyopita kuhusu mmomonyoko wa maadili katika uongozi wa juu.
Alitoa mfano namna mawaziri wanavyoamrisha makatibu wakuu kusaini fedha za Serikali kwa ajili ya matumizi binafsi ya Waziri jambo ambalo ni kinyume cha maadili. Aliwahimiza mawaziri hao ambao hawajasaini kiapo cha uadilifu kutimiza mara moja agizo hilo, kwa kuwa kiapo hicho kinamaanisha na kuahidi utumishi uliotukuka kwa wananchi.
“Kiapo hiki ni kama kujinyonga mwenyewe, ukisha saini hakuna namna lazima ufuate yale uliyoahidi mwenyewe na ndio maana nakala moja inabaki katika ofisi za sekretarieti ya maadili na nyingine anaondoka nayo kiongozi…nampongeza Waziri Majaliwa yeye alisaini ahadi yake ya uadilifu na ameitundika ofisini kwake kama nyenzo ya kumkumbusha wajibu wake kwa Watanzania,” alisisitiza.
Aidha alisema hadi sasa kuna jumla ya viongozi wa umma zaidi ya 15,000, lakini ofisi hizo za sekretarieti ya maadili zina watumishi 200 pekee.