RAIS John Magufuli amewataka watu wote waliotelekeza mashamba na viwanda walivyouziwa na Serikali, kufufua mashamba na viwanda hivyo mapema iwezekanavyo, kabla Serikali haijavinyang’anya na kuwagawia wanaoweza kuviendesha.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilieleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake njiani, wakati akisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Alisema Mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi na mashamba mengi makubwa ambayo kama waliouziwa wangeyaendeleza, yangezalisha ajira na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani na mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli alisema anaona waliouziwa mashamba na viwanda hivyo wameamua kuyatelekeza ama kubadilisha matumizi, huku wengine wakitumia rasilimali hizo kuombea mikopo katika mabenki, jambo ambalo amesema Serikali yake haitalikubali.
“Kama nilivyowaahidi wakati wa kampeni na leo narudia, wote walioamua kutumia mashamba na viwanda walivyouziwa na Serikali kwa ajili ya kuchukulia mikopo kwenye mabenki badala ya kufanya uzalishaji, wavifufue haraka, vinginevyo tutawanyang’anya,” alisisitiza Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi waliomsimamisha katika eneo la Msamvu Mjini Morogoro.
Rais Magufuli alisimamishwa na kuwasalimu wananchi wa Wami Dakawa, Magole na Dumila ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa atatekeleza ahadi yake ya kuwapa mashamba atakayonyang’anya kutoka kwa walioyatelekeza, amewataka kuachana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji na badala yake watatue migogoro hiyo kwa kutumia njia za kisheria.
Aidha, aliwataka viongozi wote wa mkoa hadi vitongoji, kushirikiana kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kabla haijasababisha madhara, na kuonya kuwa migogoro hiyo ikileta madhara, itakuwa kigezo tosha kuwa viongozi hao wameshindwa kutekeleza wajibu wao na wanapaswa kuachia ngazi.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliwahimiza wananchi hao kuchapa kazi kwa juhudi hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha, na pia wahakikishe kuwa watoto wote wanaopaswa kuandikishwa shule wanapelekwa, hasa baada ya Serikali kuamua kutoa elimu bure ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
“Tumeamua kutoa elimu bure na tutatoa elimu bure, na jambo hili limeonesha mafanikio makubwa kwa kuwa hata shule zilizotarajia kuandikisha wanafunzi 45 zimejikuta zikiandikisha hadi wanafunzi 600 kwa darasa moja,” alibainisha Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikagua kipande cha Barabara Kuu ya Morogoro - Dodoma kilichoharibiwa na maji ya mvua katika eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma na kujionea kazi za ukarabati zinazofanywa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuongeza wakandarasi wa kukarabati eneo hilo, ili kazi ikamilike haraka badala ya kusubiri mpaka baada ya miezi miwili ilivyopangwa na wizara.
Wakati huo huo, Rais Magufuli leo atashiriki maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitakazofanyika katika Uwanja wa Namfua, mjini Singida.