Bweni la wavulana la shule ya sekondari ya wavulana ya Iyunga jijini Mbeya lililoteketea.(Picha kwa hisani ya Jamiimojablog).
WANAFUNZI 95 wa shule ya sekondari ya wavulana ya Iyunga jijini Mbeya hawana mahali pa kulala baada ya moto kuteketeza bweni lao lililokuwa likifahamika kwa jina la Mkwawa.
Mkuu wa shule hiyo, Edward Mwantimwa alisema jana kuwa moto huo ulizuka majira ya saa 4:00 asubuhi wakati wanafunzi wakiwa darasani wakiendelea na masomo na baadaye askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika na kufanikiwa kuuzima ukiwa tayari umeteketeza bweni lote na kila kilichomo.
Mwantimwa alisema hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa na moto huo ingawa umeteketeza vifaa mbalimbali vikiwemo vitanda, magodoro na nguo za wanafunzi 95 waliokuwa wakilitumia bweni hilo huku bweni jirani la Nyerere likiathiriwa kidogo pia.

Akizungumzia chanzo cha tukio hilo, mkuu huyo wa shule alisema kwamba moto ulitokana na hitilafu ya umeme kwenye soketi ambayo ipo karibu na mlango lakini hakubainisha iwapo soketi hiyo ilikuwa ikitumika wakati wa tukio likitokea au la.
Alisema kutokana na moto kuanzia katika eneo la mlango ilikuwa vigumu kwa waokoaji kuweza kuingia ndani na kuokoa vitu vilivyokuwemo.
“Lakini nashukuru Mungu katika ajali hii hakuna mmwanafunzi aliyepoteza maisha zaidi ya kupoteza vitu vyao,” alisema Mwantimwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Munasa alisema kuwa tukio la moto ni la pili kutoke baada ya lile la mwaka 2003 na kwamba sababu ya moto ni n uchakavu wa miondombinu ya shule hiyo kongwe iliyojengwa tangu wakati wa utawala wa mkoloni.
Munasa alisema kutokana na uchakavu wa majengo wanafunzi pamoja na watumishi shuleni hapo wanapaswa kuchukua taadhari katika utumiaji wa miundombinu hiyo hasa ya umeme, vyoo, na maji ambayo inaokena inauchakavu mkubwa.
“Tumezunguka majengo yote na hii siyo mara ya kwanza, hata juzi nilifika hapa nikiwa na Naibu Waziri wa Elimu, Stella Mayaya. Tulizunguka na tuliona hali ya miondombinu hasa ya umeme, maji pamoja na vyoo siyo nzuri hivyo niwaombe mtumie kwa taadhari sana wakati ambao Serikali inafanya mpango kuboresha miondombinu,” alisema Nyirembe.
Mkuu huyo wa wilaya alimtaka kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mbeya, Dk Samwel Lazaro kununua vifaa muhimu kwa mahitaji wa wanafunzi wakati mpango wa kukarabati jengo la bweni lililoungua ukiendelea kufanyiwa kazi.