Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene
WAKUU wa mikoa 26 ya Tanzania Bara wamekabidhi ripoti za uhakiki wa watumishi hewa katika mikoa yao, ambazo zimeonesha kuwa na watumishi hewa zaidi ya 2,000, huku Mkoa wa Shinyanga ukiwa hauna mtumishi hewa yeyote wakati Mwanza ndio kinara ukiwa na watumishi hewa 334.
Watumishi hao zaidi ya 2,000 wameisababishia serikali hasara zaidi ya Sh bilioni nne, huku mikoa ya Mwanza, Singida, Kigoma, Pwani, Dodoma, Morogoro na Kilimanjaro ikionekana kuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa.

Ripoti hizo ziliwasilishwa jijini Dar es Salaam jana na Wakuu wa Mikoa hao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye alisema ripoti hizo atazifikisha kwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi kwa ajili ya kuhakikiwa, kabla ya kuwasilisha kwa Rais John Magufuli.
“Nitazipeleka kwa Waziri wa Utumishi ili yeye azifanyie uhakiki na zipitiwe upya…hata kwenye wizara pia ufanywe uhakiki wa watumishi hewa kwa sababu unaweza ukakuta hata wizarani wapo. Hili suala nitalifikisha kwa Waziri wa Utumishi,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa baada ya kukamilika itafikishwa mbele ya Rais Magufuli.
Aidha, aliwataka wakuu hao wa mikoa, kutambua mamlaka yao na kuyatumia ipasavyo ili kila aliyehusika kwa namna moja au nyingine katika watumishi hao hewa anachukuliwa hatua haraka ipasavyo. Awali, wakiwasilisha ripoti zao, baadhi ya wakuu wa mikoa walisema kuwa bado hawajapata idadi kamili ya fedha zilizopotea kutokana na idadi ya watumishi hewa katika mikoa yao.
Akiwasilisha ripoti yake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda alisema wamebaini kuwepo kwa watumishi hewa 270 ambao wamesababisha hasara ya Sh bilioni 1.8 katika kipindi cha mwaka mmoja. Wengine waliowasilisha na idadi ya watumishi hewa kwenye mabano ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella (334). Alisema bado hawajapata idadi halisi ya hasara kutokana na watumishi hao kulipwa mishahara.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigume aliwasilisha (231) na hawajapata gharama halisi za fedha walizochota. Mikoa mingine iliyowasilisha ripoti na idadi ya watumishi hewa kwenye mabano ni Kigoma (171) hasara Sh milioni 104.6, Pwani (150) hasara bado haijapatikana, Dodoma (139) hasara ni Sh milioni 287 kwa kipindi cha miezi sita, Morogoro (122) hasara ni zaidi ya Sh milioni 450, Kilimanjaro (111) hasara Sh milioni 281.4.
Mingine ni Tanga (104) hasara bado haijapatikana, Mbeya na Songwe (98) hasara ni Sh milioni 459.6, Mara (94) hasara Sh milioni 121, Dar es Salaam (73) hasara Sh milioni 316, Lindi (57) hasara Sh milioni 36.2, Tabora (38) hasara Sh milioni 118.7 na Ruvuma (37) hasara Sh milioni 58. Mkoa wa Simiyu (62) hasara Sh milioni 320, Njombe (34) hasara Sh milioni 20.1, Katavi (21) hasara Sh milioni 20.7, Manyara (50) hasara Sh milioni 42, Iringa (15) hasara haijapatikana na Kagera (14) hasara Sh milioni 49.1.
Akitoa siri ya mkoa wake kutokuwa na watumishi hewa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela alisema viongozi waliotangulia kabla yake, waliweka mikakati mizuri jambo lililowezesha wasiwepo watumishi hao. “Viongozi waliokuwepo walianza zoezi hili tangu mwezi Julai mwaka jana na kila tarehe 26 ya mwisho wa mwezi walikuwa wakihakiki watumishi wao hivyo ndio maana hakuna watumishi hewa,” alisema Anne- Kilango, ambaye katika Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema katika mkoa wake yapo majina ya watumishi hewa, ambayo yapo katika orodha ya malipo ya mishahara, na kutoa mfano wa Manispaa ya Tabora peke yake hasara iliyotokana na kulipa watumishi hewa ni Sh milioni 24. Machi 15, mwaka huu wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa, Rais Magufuli alitoa siku 15 kwa viongozi hao kuhakikisha wanajumuisha wafanyakazi wote na kuwaondoa watumishi hewa.
Aidha, juzi Rais Magufuli alisema uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa nchini, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa Sh bilioni 1.8. Alisema ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima, utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za Watanzania.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Chato mkoani Geita juzi, Rais Magufuli alitoa mfano wa mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo atafikishwa mahakamani. Awali akifungua kikao cha kujadili bajeti inayopelekwa bungeni na utekelezaji wa bajeti iliyopita, Waziri Simbachawene aliwaagiza Wakuu wa Mikoa hao kuhakikisha wanasimamia vizuri elimu bila malipo.
“Lakini pia hakikisheni watumishi wanajituma na kuwafundisha wanafunzi vizuri ili kupata elimu bora. Kuna malalamiko mengi ya wananchi ambayo yanafika mpaka kwa Rais na baadaye ndio yanarudi kwa waziri na mkuu wa mkoa, tujitahidi kuhakikisha tunatatua migogoro katika hatua ya mwanzo,” alisema Simbachawene.
Aidha, aliwaagiza kushughulikia tatizo la mlundikano wa watumishi katika maeneo ya mijini kwani mlundikano huo hauna tofauti na watumishi hewa. Alisema kwa kada ya ualimu zipo shule ambazo zina idadi kubwa ya walimu kuliko mahitaji.
“Unakuta shule moja walimu wanaotakiwa ni 40 tu lakini unakuta 120 hadi wengine hawana kazi…kisingizio ni kwamba hela ya uhamisho wahamisheni sisi tutatoa hela ya uhamisho,” alisema Simbachawene. “Serikali za Mitaa katika maeneo yenu zizingatie kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, serikali imejipanga kuhakikisha inapunguza gharama za kujiendesha kwa kubana matumizi katika maeneo yasiyokuwa na tija,” aliongeza Simbachawene.
“Mamlaka zote zinasimamia jambo la ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha ukusanyaji huo unafanyika kwa njia ya elektroniki, ambao unaonesha matokeo mazuri ni lazima uwe umeunganishwa katika mfumo wetu kwa sababu wapo watu wana zile mashine lakini hazijaungwa katika mfumo wetu,” alisema.