NapeWaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Na Idd Mumba, RISASI Mchanganyiko
MWANZA: Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaka kupewa maelezo maalum ya kimaandishi juu ya mwenendo wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Rose Muhando ili aweze kuchunguza madai ya utapeli yanayosemwa juu yake.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa endapo atafanyia kazi tuhuma zilizotolewa na waandaaji wa Tamasha la Pasaka la kila mwaka, Msama Promotions, waliodai mwimbaji huyo hakutokea jukwaani, licha ya kupewa malipo yake na stahiki zingine zilizostahili.

rose_muhandoMwimbaji wa nyimbo za Injili, Rose Muhando.
“Kwanza ieleweke kuwa mimi sikuambiwa, ila nilisikia wakiwatangazia watu waliokuwepo uwanjani juu ya kutokuwepo kwa Rose kwenye tamasha hilo. Sasa mimi siwezi kufanya kazi kwa maneno ya mtaani, kama kuna wasanii wanatapeli, niletewe maelezo kimaandishi yakiwa na ushahidi wa tuhuma zao, hapo ndipo nitaweza kujua hatua za kuchukua,” alisema.
Awali, ofisa mmoja wa Msama Promotions aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa siyo msemaji, alisema Rose alikuwa amepewa malipo yote, ikiwa ni pamoja na usafiri wa gari la kumtoa Dodoma hadi Mwanza, lakini hakuweza kutokea katika onesho hilo.
“Tulishamalizana na Rose na kila mmoja alijua atakuwepo, lakini tunashangaa mara ya mwisho hapatikani kwenye simu na hatujui kapatwa na masaibu gani,” alisema ofisa huyo.
Gazeti hili lilijaribu kumtafuta mwimbaji huyo nyota ili atoe ufafanuzi wa madai hayo, lakini simu yake ya mkononi haikupatikana. Rose Muhando ni miongoni mwa wasanii ambao wanasimamiwa na Alex Msama, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo.