Papa Wemba
Mwanamuziki nguli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba maarufu kwa jina la Papa Wemba amefariki dunia leo baada ya kuanguka akitumbuiza jukwaani nchini Ivory Coast.

Taarifa zimeeleza kuwa Wemba aliyekuwa na umri wa miaka 66 amefariki kwa shambulio la moyo baada ya kuanguka akitumbuiza jukwaani huko Abidjan nchini Ivory Coast.
Paris, FRANCE: Congolese singer Papa Wemba performs during a concert at the New Morning, 15 February 2006 in Paris. AFP PHOTO PIERRE VERDY (Photo credit should read PIERRE VERDY/AFP/Getty Images)
Historia ya Papa Wemba
PapaWemba  alizaliwa Juni 14, 1949 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.  Hadi kifo kinamkuta leo, Aprili 24, jijini Abidjan, Ivory Coast, alikuwa bado anaendeleza ‘libeneke’ la muziki ambalo lilimfanya kujulikana kama ‘Mfalme wa Rhumba’.
Papa Wemba ambaye amefariki baada ya kuanguka jukwaani wakati akitumbuiza huko Ivory Coast usiku wa kuamikia leo, ni mmoja wa wanamuziki wa Congo (Kinshasa) waliovuma zaidi ndani na nje ya mipaka ya nchi yake, Afrika na Ulaya.
Kwa walioanza kumfahamu mapema ni pale alipokuwa katika bendi maarufu nchini mwake iliyokuwa imebatizwa jina la ‘Bendi ya Vijana’ ya Zaiko Langa Langa (Nkolo Mboka) ambayo iliwavutia wapenzi wengi wa muziki, wakati huo ikiwa imejaa majina ya wanamuziki wengi  mahiri wakiwemo kina  Nyoka Longo Jossart, Manuaku Pepe Felly, Evoloko Lay Lay, Bimi Ombale, Teddy Sukami, Zamuangana Enock, Mavuela Simeon, Clan Petrole na wengine.
Wembaa
Papa Wemba akitumbuiza kwa mara ya mwisho kabla ya kuanguka jukwaani usiku wa kuamkia leo.
Baada ya kujenga jina lake katika bendi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1969 jijini Kishasha, mwanamuziki huyo ambaye kabla ya kuchukua majina ya ‘kibantu’ alikuwa anajulikana kama Jules Presley Shungu Wembadio,  aliungana na wanamuziki kadhaa wakiwemo Evoloko Lay Lay, Mavuela Somo na Bozi Boziana kuanzisha kundi  lililojulikana kama Isifi Lokole mwaka 1974.
Mnamo Julai 1975,  mwimbaji huyo aliyekuwa na sauti nyembamba ya kuvutia, licha ya umbo lake, alibadili tena jina lake na kuanza kujiita Papa Wemba, jina ambalo lilijulikana sehemu kubwa katika macho na masikio ya wapenzi wa muziki, hususan soukous.
wemba 2Wemba akipatiwa huduma ya kwanza mara baada ya kuanguka jukwaani.
Katika kutafuta maslahi zaidi kimuziki, Papa Wemba akiwa na Mavuela Somo na Bozi Boziana, waliiacha Isifi Lokole na kuanzisha Yoka Lokole ambayo ilivuma kiasi kuliko Isife Lokole, lakini bado iliweza kumjenga zaidi kutokana na vibao alivyovitoa kama vile  “Matembele Bangui”, “Lisuma ya Zazu” (Papa Wemba), “Mavuela Sala Keba”, na “Bana Kin” (Mavuela Somo).
Mwaka 1977 alianzisha tena kundi la Viva la Musica ambalo liliendeleza umaarufu wake ndani na nje ya nchi hiyo na nje na kumfanya kutumbuiza katika nchi mbalimbali duniani kwa mafanikio makubwa na baadaye kushirikiana na wanamuziki wengine katika fani hiyo.
Pamoja na matatizo mbalimbali ya kibinafsi na kimuziki, Papa Wemba aliendelea kulitumia jukwaa la muziki kama ‘mkate’ wake wa kila siku hadi mauti yalipomfika leo, akiwa katika harakati za kutumia muziki kuupata ‘mkate’ wake.
Miongoni mwa nchi alizowahi kutembelea duniani ni pamoja na Tanzania ambapo alikuja kutokana na mwaliko wa kampuni East African Television (EATV) iliyo chini ya makampuni ya IPP, mnamo miaka ya 1990.
Wapenzi wa muziki duniani, ni dhahiri wataikosa sauti yake nyororo ambayo, miongoni mwa vibao vikali alipoionyesha ni katika wimbo wa ‘Show Me The Way’!
Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.  Amen!
Video: Hivi ndivyo Papa Wemba alivyoanguka jukwaani.