Mahakama mjini Kigali imeanza kusikiliza kesi ya rufaa iliyowasilishwa na kundi la waislamu wakipinga kifungo cha muda katika kesi inayohusu ugaidi.
Kundi hilo linatuhumiwa makosa ya kuhamasisha na kusajili wapiganaji wa kujiunga na kundi la IS nchini Syria.
Watuhumiwa 11 miongoni mwa 17 ndio wamejitokeza mahakamani.
Kinyume na ilivyokuwa awali usalama haukuwa mkali kiasi kwamba watuhumiwa waliweza kuongea na jamaa zao waliokuwepo kuwaunga mkono.
Washtakiwa na mawakili wao walitaka mahakama kupinga uamuzi uliochukuliwa na mahakama ya mwanzo wa kuwapa kifungo cha muda cha siku 30 badala yake wakataka kesi yao isikilizwe wakiwa nje ya kizuizi.
Hakuna mengi yaliyosikilizwa kwani kabla ya hoja za kesi hiyo kuendelea,mwendesha mashitaka ameomba mahakamani kesi hiyo isikilizwe kwa faragha.
Jaji ameunga mkono ombi hilo na kuwataka waliohudhuria kesi kutoka nje isipokuwa washitakiwa na mawakili wao.
Katika kesi ya awali,watuhumiwa walikana mahusiano ya aina yoyote na kundi la Islamic State na kwamba kamwe hawajashiriki mafunzo yoyote ya kijeshi kwa lengo la kusaidia kundi hilo kama yalivyo mashitaka dhidi yao.
Mahakama ya mwanzo ilikuwa imechukua uamuzi wa kuwaweka kizuizini kwa muda ikizingatia ushahidi wa marehemu Imam Mohamed Mugemangango aliyeuawa mwezi wa kwanza mjini Kigali kwa kupigwa risasi na polisi kwa madai kuwa alitaka kutoroka.
Imetangazwa kwamba katika ngazi Imamu huyo alikuwa ametangaza kuwa watuhumiwa hao ni kundi linalotafuta vijana wa kujiunga kundi na Islamic State na wako tayari kufanya Jihad.
Lakini wao wanasema ushahidi wa mtu aliyekufa hauwezi kuzingatiwa.
Kesi itaendelea kusikilizwa kwa faragha.
|
0 Comments