Rais Dkt John Magufuli akigonganisha glasi na Rais Paul Kagame wa Rwanda
RAIS Paul Kagame wa Rwanda amempongeza na kumsifia Rais John Magufuli kutokana na mfumo wa uongozi wake hasa nia yake thabiti ya kupambana na ufisadi.
Kagame aliyasema hayo juzi katika hafla ya chakula cha jioni aliyoiandaa kwa ajili ya mgeni wake, Rais Magufuli aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili katika taifa hilo .

“Kwanza nataka ujue kuwa hapa ni nyumbani kwa kaka yako. Tangu uchaguliwe kuwa Rais, uwepo wako umekuwa wa kipekee, matendo na maneno yako yanaakisi maono yetu,” alisema Rais Kagame.
Aidha, alisema jitihada na msimamo wa Dk Magufuli katika kupambana na tatizo la rushwa na ufisadi ni wa kupongezwa na kuigwa.
Akiwasili nchini humo juzi, Dk Magufuli alisafiri umbali wa takribani kilometa 1,460 kwa barabara, ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi nje ya Tanzania tangu achaguliwe kushika wadhifa huo Oktoba mwaka jana.
Msafara wa Rais huyo ulipokewa kwa shangwe na wananchi wa Rwanda wakati ukipita kwenye mji wa Rusumo kwenda mpakani mwa nchi ya Rwanda na Tanzania.
Baada ya kuwasili Rusumo ambako ni mpaka wa Tanzania na Rwanda katika wilaya ya Ngara kwa Tanzania, Dk Magufuli na mwenyeji wake walifungua majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpak ani kilichopo upande wa Tanzania, kisha wakafungua daraja la mto Kagera.
Dk Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli jana waliungana na wananchi wa Rwanda kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari yaliyosababisha vifo vya watu takribani milioni moja.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika eneo la Gisozi mjini Kigali yalipo makumbusho ya mauaji ya Kimbari ambako Rais Magufuli na mkewe wakiwa na mwenyeji wao Rais Paul Kagame na mkewe Mama Janeth Kagame waliweka shada la mau katika eneo walipouawa idadi kubwa ya wananchi wa Rwanda na pia wakawasha mwenge wa matumaini kwa walionusurika katika mauaji hayo na kwa Taifa zima la Rwanda.
Pamoja na kupata historia ya mauaji hayo ya kimbari, Rais Magufuli akiongozwa na mwenyeji wake alitembelea jumba maalumu lililohifadhi kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha, ambako alipata maelezo kutoka kwa wahifadhi wa makumbusho hiyo, na pia kujionea picha na mabaki ya mifupa na mafuvu ya binadamu waliouawa.
Akizungumza baada ya kutembelea jumba hilo la makumbusho, Rais Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na mauaji hayo na kusema tukio hilo halipaswi kurudia.
“Haitatokea tena, hatuwezi kubadilisha yaliyopita lakini tunaweza kubadilisha mambo ya sasa na yajayo, mauaji haya hayapaswi kutokea tena,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ambaye aliingia nchini Rwanda juzi ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana, aliondoka Kigali jana jioni na kurejea jijini Dar es Salaam.