|
MZIMU umeendelea kumwandama Mbunge wa Mvomero, Suleiman Saddiq Murad baada ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuzifungia kwa muda usiojulikana tanuri mikate nne zilizopo katika Manispaa ya Morogoro, ikiwemo inayomilikiwa na mbunge huyo kwa kushindwa kutimiza masharti ya viwango vya ubora.
Tanuri mikate hizo zilikaguliwa kwa mara ya kwanza Julai mwaka jana na wamiliki wake kupewa muda wa miezi sita kurekebisha kasoro zilizokuwepo, lakini hadi Machi 10, mwaka huu katika ukaguzi mwingine walikuwa hawajatekeleza na kutimiza masharti yaliyotolewa na TBS.
Mkaguzi wa TBS, Ashura Katunzi alisema kazi ya kuzifungia tanuri mikate hizo ipo kisheria baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata utaratibu walioelekezwa awali wa kurekebisha kasoro kabla ya kuanza kwa uzalishaji tena.
Katunzi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora wa TBS, alisema: “Kabla ya kufunga bekari hizi, wakaguzi wa TBS walizitembelea tena mnamo Machi 10, mwaka huu ili kujiridhisha na iwapo utekelezaji umefanyika katika kipindi cha miezi sita waliopewa, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema Katunzi juzi wakati wakifanya ukaguzi na kuchukua uamuzi huo.
Alisema kutokana na kukaidi agizo hilo, TBS imezifungua kwa muda usiojulikana hadi watakaporekebisha kulingana na maelekezo na kuomba upya kufunguliwa baada ya ukaguzi mwingine kufanyika.
Tanuri mikate zilizofungiwa kuanzia juzi ni MS Bakery Magooma Super Market inayomilikiwa na Murad, Baraka Bakery mali ya Salim Nassor, Sifasita Bakery inayomilikiwa na Tanzua Tambi na M&M Bakery mali ya Sarah Sanya.
“Bekari hizi zimekutwa zinafanya kazi katika mazingira hatarishi yasiyo salama na yanatia hofu kwa mlaji, zina ukosefu wa vyoo, zipo kwenye makazi ya watu na ukosefu wa vyumba vya kubadilisha nguo kwa wafanyakazi,” alifafanua Katunzi na kuongeza: “Katika ukaguzi wetu tumeona bekari hizi zina ukosefu wa eneo maalumu la kuoshea vyombo, uchakavu wa sakafu, mikate kuwekwa sakafuni na ufinyu wa eneo la kazi.”
Alisema endapo wamiliki hao watarekebisha kasoro na kutimiza viwango vya ubora, wanatakiwa kuwasilisha tena maombi rasmi TBS ili wakaguliwe tena ili kujiridhisha iwapo wametimiza vigezo kabla ya kufunguliwa tena.
“Watakapoharakisha kufanya marekebisho waliyoelelezwa, ndipo watakapoweza kufunguliwa haraka kuendelea na uzalishaji tena,” alifafanua mkaguzi huyo wa shirika la viwango.
Naye Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema licha ya kuzifungia tanuri mikate hizo, kazi hiyo inaendelea ili kuzifikia nyingine zilizokaguliwa na kushindwa kutekeleza masharti yake.
Hivyo alitoa mwito kwa wazalishaji wa mikate katika Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine wafuate utaratibu na kuweka ubora wa mikate kwa kuzingatia viwango vya TBS kabla ya kufikisha sokoni kwa walaji.
Baadhi ya wafanyakazi waliokutwa katika tanuri mikate hizo waliwasihi wakaguzi wa TBS wasiwafungie na badala yake wawapatie muda wa ziada ili warekebishe kasoro hizo wakati wakiendelea na uzalishaji, maombi yaliyogonga mwamba kutokana na kufungwa kwa milango kwa makomeo chini ya ulinzi wa Polisi.
0 Comments