RAIS John Magufuli amekamilisha kutengeneza muundo wa serikali yake na anatarajiwa kutangaza muundo huo katika Gazeti la Serikali (GN) muda wowote kuanzia sasa.
Kutokana na kukamilika kwa muundo huo, Rais ameshatoa maelekezo ya utendaji kwa mawaziri wote na viongozi wengine kulingana na muundo wa serikali yake na hivyo wanatekeleza majukumu yao kutokana na maelekezo ya Rais.
Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa anatoa majumuisho ya hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017.
Waziri Mkuu alisema baada ya kuapishwa, Rais alianza kazi ya kuunda serikali yake kwa kuteua mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine, kazi aliyoendelea kuifanya hadi hivi Aprili 20, mwaka huu alipoikamilisha.
Alisema tofauti na magazeti la kawaida, GN hutolewa baada ya kukamilika kujengwa kwa hoja juu ya suala husika na ndio maana isingekuwa vema kwa Rais kutoa tangazo hilo wakati akiendelea kuunda serikali yake.
“Napenda sasa kuliarifu Bunge kuwa Rais atatangaza kwenye GN muundo wa serikali yake wakati wowote kuanzia sasa, na kwa maana hiyo Mawaziri wote na viongozi wengine wa juu wa serikali wanafanya kazi kwa maelekezo ya Rais, lakini pia kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Hoja kwamba serikali iliyopo madarakani haipo kihalali kutokana na kutotangazwa kwa muundo wa serikali katika Gazeti la Serikali, iliibuliwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, na kusema ni moja ya sababu zilizoifanya kambi hiyo kususa hotuba hiyo ya Waziri Mkuu.
Bunge jana lilipitisha bajeti hiyo ya Waziri Mkuu, huku wabunge 93 wakiwa wamepata nafasi ya kuijadili, wabunge 80 wakichangia kwa maneno bungeni, na wengine 13 wakiwa wamechangia kwa maandishi.
Kabla ya kujibu hoja zilizojitokeza kwenye mjadala wa hotuba yake, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa pole kwa wananchi waliokumbwa na maafa ya mafuriko katika wilaya za Rombo, Moshi Vijijini na Kilosa.
|
0 Comments