SHILINGI trilioni 107 zinahitajika kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/21, ambao utategemea sana makusanyo ya kodi na ukijikita katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.
Akiwasilisha bungeni jana Mpango huo wa Pili wa Maendeleo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alisema katika fedha hizo, Sh trilioni 59 zitatolewa na serikali, huku kiasi kilichobaki cha Sh trilioni 48 zitachangiwa na sekta binafsi pamoja na mikopo na misaada kutoka nje.
Akitoa mchanganuo wa ugharamiaji mpango huo, Dk Mpango alisema kila mwaka serikali itatoa Sh trilioni 11.8 na kwamba katika kipindi cha miaka mitano ya mpango huo, serikali itakuwa imetoa jumla ya Sh trilioni 59.
Alisema eneo la pili la gharama za mpango huo, litabebwa na sekta binafsi, mkopo na misaada kutoka nje na kuwa serikali inaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya maendeleo.
Alisema katika mpango huo, kuna ongezeko kubwa la fedha za kugharamia mpango huo, ukilinganisha na ule wa kwanza na sababu ya ongezeko hilo ni ukubwa wa miradi tarajiwa sambamba na ni ya kuchochea upatikanaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji.
Alisema nchi ikiwekeza kwenye ujenzi wa viwanda, huvutia misaada kutoka nje na hiyo imetokana na uzoefu wa nchi nyingine zilizoweka mikakati kwenye uwekezaji wa viwanda. “Mantiki yetu ni kwamba nchi haina budi kuwa na mkakati mahususi wa kukusanya fedha kuwezesha utekelezaji wa mpango huu kwa ufanisi,” alisema Dk Mpango.
Kwa upande wa serikali, Dk Mpango alisema fedha za kugharamia mpango huo, watazipata kwenye makusanyo ya kodi na yale yasiyo ya kodi, ambapo serikali imeainisha miradi mikubwa ya kielelezo kama ile ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga.
Aidha, eneo jingine ni ujenzi wa Reli ya Kati na kuboresha miundombinu mingine, zikiwemo barabara na usafiri wa anga. Hata hivyo, Dk Mpango alisema katika eneo ya kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu, bado kiwango cha umaskini nchini ni kikubwa.
Alisema hivi sasa nchini kuna watu maskini zaidi ya milioni 10, idadi ambayo ni kubwa kuliko baadhi ya nchi Afrika na kusema Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2016/17 hadi 2021, umelenga kupunguza kiwango hicho.
Dk Mpango alisema hatua hiyo inatokana na ule mpango wa kwanza 2011/16 kufikia ukomo wake ifikapo Juni mwaka huu huku kukiwa bado na changamoto nyingi. Alisema pamoja na mpango unaoisha muda wake kutekelezwa kwa kiasi, lakini bado zipo changamoto kubwa zinazopaswa kupewa kipaumbele katika mpango huo mpya ili kuhakikisha jitihada zinawekwa katika kuleta maendeleo ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
“Tanzania ina watu maskini zaidi ya milioni 10, idadi hii ni kubwa kuliko baadhi ya nchi barani Afrika na idadi hii haishiriki kikamilifu katika uzalishaji, kaya nyingi zimebeba mzigo mkubwa wa wategemezi kufuatia kasi kubwa ya kuzaliana na athari za magonjwa yakiwemo Ukimwi,” alieleza Dk Mpango.
Aidha, aliongeza changamoto nyingine inayoongeza kasi ya umaskini wa watu ni ukosefu wa ajira na kwamba kati ya vijana 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza masomo, ni 200,000 ndio wanaobahatika kupata ajira katika sekta rasmi. Hivyo mpango huo wa maendeleo kwa mwaka 2016/17 umelenga kuongeza kasi ya ukuaji uchumi kwa kuhakikisha unaongezeka kutoka asilimia 7.0 ya mwaka 2015 hadi kufika asilimia 10 ifikapo mwaka 2020.
Aidha, mpango huo umelenga kuongeza pato la wastani kwa kila mwananchi kutoka Dola 1,006 kwa mwaka 2015 hadi kufikia Dola 1,500 ifikapo mwaka 2020 na pia kuhakikisha mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani yanaongezeka kutoka asilimia 24 mwaka juzi hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.
Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2016/17, umeweka vipaumbele vikuu vinne vilivyolenga ukuzaji viwanda kwa lengo la kuifanya nchi itimize malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Vipaumbele hivyo ni kuwa na viwanda vya kukuza uchumi, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kipaumbele cha nne ni kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Katika vipaumbele hivyo, sekta zote zitaangaliwa na kuwekewa mikakati ya kuziboresha ikiwemo viwanda, kilimo, afya, elimu, miundombinu, rasilimali watu kwa kuhakikisha nchi inafikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Katika utekelezaji huo, viwanda vilivyokufa na vile visivyoendeshwa kwa tija vitafufuliwa na vingine kuanzishwa ili visaidie kuongeza uzalishaji wa mazao yenye thamani na kukuza kipato cha watanzania na taifa kwa ujumla.
Aidha, Dk Mpango amewaasa Watanzania kuacha na kuukana utamaduni wa kuishi maisha ya kipato wasichoweza kukimudu na badala yake wafanye mageuzi ya mfumo wa maisha kwa kujizatiti kuzalisha mali huku serikali ikiweka nguvu kwenye ukusanyaji mapato ya kodi na yale yasiyo ya kodi.
Akihitimisha hotuba yake hiyo bungeni, alisema hakuna budi kwa Watanzania kubadilika na kubadilisha mfumo wa maisha. “Desemba 9, mwaka huu tutaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa nchi yetu, maana yake ni kuwa kiumri nchi yetu si changa tena, ina umri wa mtu mzima anayepaswa kuwa na familia na uwezo wa kujitegemea kimaisha, hatupaswi kuwa wategemezi, sharti tujijenge,” alisema Dk Mpango.
Alisema katika hilo hakuna njia ya mkato na kwamba nchi inapaswa kujizatiti kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kutoka vyanzo vyetu vya ndani kwa nguvu zote na kuacha matumizi ya starehe.
Dk Mpango alisema matumizi ya starehe katika maisha ya sasa na ya uchumi wa nchi hayapaswi kuendekezwa na Watanzania, ikiwa wanataka kuondokana na umaskini na utegemezi wa kibajeti.
Akisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondokana na umaskini na kuwasaidia wananchi kuzalisha mali hivyo vita vya mageuzi ya mfumo wa maisha ni lazima ufanywe kuanzia ngazi ya familia ili kuishi maisha ya kipato wanachoweza kukimudu na sio kuisha maisha ya ufisadi.
“Ndio sababu Rais Dk John Magufuli amekuja na kauli ya kutumbua majipu inayoendelea na ni dhana nzuri ya kukubali tiba kwa kuwa wapo wengi miongoni mwetu watajitahidi kukataa kupokea maumivu haya, japo hii ndiyo njia pekee ya kupona,” alisema Dk Mpango.
Akizungumzia ukuaji wa uchumi kwa kuwekeza kwenye viwanda, alisema hiyo ndiyo njia ya uhakika kufikia maendeleo endelevu inayotumiwa na nchi nyingi duniani na Tanzania imeamua kujipanga upya kiuchumi kufikia huko.
“Ni dhahiri katika njia hii kutakuwa na vikwazo pamoja na ushindani katika masoko ya mitaji ya bidhaa, ila ili tuvuke tunahitaji dhamira ya dhati kuibadilisha nchi yetu kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi kwa wananchi wote,” alisema Dk Mpango.
|
0 Comments