Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
SERIKALI iko katika hatua ya mwisho ya kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ambaye ni mtu sahihi na mwenye uwezo mkubwa wa kusimamia na kuendesha bandari hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, tayari majina manne yameshawasilishwa na yanafanyiwa kazi ili kuteua jina la mmoja atakayeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA

Profesa Mbarawa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili mkoani Kigoma, ambako alikutana na wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena.
Akijibu risala ya wafanyabiashara na wasafirishaji hao, Profesa Mbarawa aliitaka TPA na Mamlaka ya Mapato (TRA) kufanya kazi siku za mwishoni mwa wiki na sikukuu ili kuhudumia shehena za wafanyabiashara wanaotaka kusafirisha mizigo yao kwenda nje ya nchi ili kuwafanya watumie siku chache katika usafirishaji wa shehena zao.
Katika risala yao, wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena walilalamikia urasimu wa mamlaka hizo unaofanya wafanyabiashara kutumia siku nyingi kusafirisha shehena zao na hivyo kusababisha kuwepo kwa ongezeko la gharama katika usafirishaji wa shehena hizo wanapotumia Bandari ya Kigoma.
Hata hivyo, TPA katika warsha ya siku mbili kwa Wahariri wa Habari wa vyombo mbalimbali nchini iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, ilisema bandari inafanya kazi saa 24 na kwamba kama nyaraka zote zinazohitajika kutoa mzigo zinapatikana kwa muda mwafaka, mzigo unatolewa ndani ya muda wa siku 0.2.
“Katika ushindani wa biashara uliopo sasa baina yetu na wenzetu wa nchi nyingine hatuna budi kufanya kazi kwa tija na ufanisi mkubwa ili kuwalinda wateja wetu wasiweze kukimbia na kufanya kazi mwishoni mwa juma na siku za sikukuu kama kuna shehena ya kupakia na kupakua bandarini ni jambo la msingi sana katika kuwalinda wateja,” alisema Profesa Mbarawa.
Awali akisoma risala ya wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena, msafirishaji shehena kwenda nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Kassim Zaidi alisema urasimu wa Kampuni ya Reli (TRL) kutumia siku nyingi kusafirisha behewa zenye mzigo kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma na urasimu wa TRA na TPA umewakimbiza wafanyabiashara na wasafirishaji kutumia Bandari ya Kigoma na hivyo wengi wao kusafirisha shehena zao kwa njia ya barabara.
Alisema imekuwa ikichukua zaidi ya siku 15 kwa behewa zenye shehena kutoka Dar es Salaam kufika Kigoma na wakati mwingine treni ikisimama njiani katika baadhi ya mikoa kwa siku nyingi bila sababu yoyote hali ambayo imefanya wasafirishaji wa shehena kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutumia njia nyingine za usafirishaji kutumia barabara na bandari za nchi nyingine kuepuka usumbufu.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, hadi kufikia Desemba mwaka jana, tani milioni 14.8 zilipita katika bandari hiyo, lakini ni asilimia 0.01 pekee ndiyo zilizosafirishwa kwa njia ya reli na asilimia 99.9 kwa barabara, kutokana na uchakavu wa reli na usafiri wake kutokuwa wa kuaminika.
Naye Zaidi alisema kwa waziri kuwa wamekuwa wakilalamikia vitendo vya baadhi ya watumishi wa TRA na TPA kukataa kufanya kazi Jumamosi na Jumapili wakitaka kulipwa posho ya kufanya kazi ya ziada na msafirishaji wa shehena badala ya ofisi zao, hali aliyosema inawaingiza wasafirishaji gharama kubwa za kuuhifadhi mzigo huo.