SERIKALI ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi kwa nguvu zote bila kutetereka.
Lengo la hatua hiyo ni kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuboresha uwajibikaji na maadili katika usimamizi wa rasilimali za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema hayo katika hotuba yake kwa Taifa wakati wa sherehe ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Hivyo aliwaomba Watanzania wote kuunga mkono kwa vitendo juhudi na maelekezo ya Dk Magufuli za hatua anazozichukua dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi nchini. Kutokana na hatua hizo, Makamu wa Rais alisema hadi sasa jumla ya kesi 596 za rushwa zinaendelea mahakamani na jumla ya Sh 6,543,342,793 tayari zimeokolewa.
“Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha Watanzania wenzangu kujiepusha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa,” alisema Samia na aliwataka watumishi wa umma, watumishi katika sekta binafsi, wajasiriamali na kila mmoja kujiepusha na vitendo vya rushwa na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa.
“Kama nilivyokwishasema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya Rushwa chini ya kaulimbiu “Timiza Wajibu wako, kata Mnyororo wa Rushwa,” aliongeza Makamu wa Rais.
Samia alisema suala la rushwa limeongelewa mara nyingi na athari zake zinajulikana ikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa mali za umma, mikataba isiyofaa kwa taifa na udanganyifu na kupokea fedha ili kukiuka sheria kwa manufaa binafsi huchangia kwa kiwango kikibwa kuwanyima wananchi hazi zao na kudhoofisha ustawi wa taifa letu.
Mbali na hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendelea na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pia alisisitiza kwa mara nyingine kwa kusema kuwa Serikali haina nia ya kumwonea mtu inapochukua hatua ya kutumbua majipu kwa watumishi wa umma.
Akishangiliwa na wananchi wakati akiwahutubia kwenye sherehe hizo, Makamu wa Rais alisema lengo la Serikali la kutumbua majipu ni kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji serikalini kama ilivyoagizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili Watanzania wote wafaidike na matunda ya nchi yao.
“Mnasikia katika Serikali ya Awamu ya Tano tunarekebishana, majipu yanatumbuliwa ...kwa kweli hatuna nia ya kumwonea mtu, tunarekebishana na hilo ndilo lililomo katika agizo ya Ilani yetu ya CCM ili kuwanufaisha Watanzania wote wafaidi matunda katika nchi yao,” alisema Makamu wa Rais.
|
0 Comments