WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 30. Wabunge hao ni Mbunge wa Mvomero, Ahmad Saddiq (53), Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (54) na wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63).
Walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka yao na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Emmanuel Jackob akisaidiwa na Maghela Ndimbo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hata hivyo, washitakiwa walikana mashitaka, na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja, kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano na kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini hati ya kiasi hicho.
Awali, akisoma mashitaka, wakili Jackob alidai kuwa, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka moja la kujihusisha na rushwa. Alidai Machi 15 mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne usiku katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa kama wabunge na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta.
Inadaiwa wabunge hao waliomba kiasi hicho cha pesa, kama kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa walikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo, unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Simba aliutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha wanakamilisha upelelezi haraka ili kesi ianze kusikilizwa. Aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 14 mwaka huu itakapotajwa tena. Washitakiwa wapo nje kwa dhamana.
Akizungumza baada ya kutoka mahakamani, Lugola alisema licha ya vita ya kisiasa vinavyoendelea, wapo ‘ngangari’ na wataendelea kutumbua majipu. Kashfa ya wabunge hao kuhusishwa na rushwa, iliibuka siku chache zilizopita.
Tayari Spika wa Bunge Job Ndugai, amefanya mabadiliko katika baadhi ya kamati za Bunge. Hata hivyo, Ndugai alisisitiza kuwa mabadiliko aliyofanya, yalizingatia mahitaji mapya na changamoto mpya zilizojitokeza baada ya kuunda Kamati hizo Januari mwaka huu.
Pamoja na madai hayo, mabadiliko hayo ya kamati yaligusa takribani wenyeviti na makamu wenyeviti wote, wanaotuhumiwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine na vitendo vya rushwa kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku (si HabariLeo).
Wenyeviti wanaotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Sumbawanga Aeshi Hilaly na wabunge wa Viti Maalum, Martha Mlata na Dk Mary Mwanjelwa.