RAIA wawili wa China wamehukumiwa kifungo cha miaka 11 jela au kulipa faini ya Sh milioni 50 kila mmoja, kwa kosa la kusafirisha Sh milioni 20 kwenda nchini China bila kibali kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha baada ya washtakiwa kukiri kosa. Washtakiwa waliohukumiwa kifungo hicho ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Feng Shi Trading, Sun Ning (39) na Fen Quan (51).
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha alisema washitakiwa wamepatikana na hati ya makosa matatu, na kwa kosa la kwanza kila mmoja atalipa faini ya Sh milioni 10 au kutumikia kifungo cha miaka mitano jela, kosa la pili faini ya Sh milioni 20 au jela miaka mitano, kosa la tatu faini ya Sh milioni 20 au jela mwaka mmoja.
Alisema kwa makosa yote, adhabu yao ni sawa na kifungo cha miaka 11 jela au kila mmoja kulipa faini ya Sh milioni 50, lakini adhabu ya kifungo inakwenda sambamba hivyo ni sawa na kifungo cha miaka mitano jela.
Hakimu Mkeha alisema ametoa adhabu hiyo kwa kuzingatia kuwa, washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na wamekuwa na ushirikiano mzuri kwa kukiri makosa yao kwa madai walikuwa hawajui kama ni kosa.
Aidha alisema kwa sababu fedha hizo hazijafanikiwa kuhamishwa na zilikuwa fedha halali za washtakiwa hao, aliamuru Sun arudishe fedha zake Sh milioni 20. Katika mashtaka yao inadaiwa kati ya Agosti 15 na 31 mwaka jana, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Ilala Dar es Salaam, washtakiwa hao walisafirisha noti 10,000 za Sh 500 zenye thamani ya Sh milioni tano kwenda China bila kibali kutoka kwa gavana.
Aidha wanadaiwa kati ya Desemba 22 na 31 mwaka jana wakiwa uwanjani hapo, walisafirisha noti 10,000 za Sh 500 zenye thamani ya Sh milioni tano bila kibali, pia walikutwa wakisafirisha noti 40,000 za Sh 500 za thamani ya Sh milioni 20 kwenda China bila kibali.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washtakiwa hao walikiri kutenda kosa hilo na kusomewa maelezo ya kesi ambapo ilidaiwa kwamba Sun ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Feng Shi Trading aliingia nchini Machi 13 mwaka huu.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali, Machi 10 mwaka huu Feng alitoa noti za 500 zenye thamani ya Sh milioni 20 kutoka kwenye akaunti yake namba 015240837900 CRDB Tawi la Kariakoo.
Ilidaiwa baada ya kuchukua fedha hizo, Sun alimpa Feng dola za Marekani 8,120 na yeye kumpa fedha hizo za Kitanzania na Machi 14 mwaka huu Feng aliingiza dola 8000 katika akaunti yake ya fedha za kigeni iliyopo benki ya CRDB.
Machi 16 mwaka huu Feng alimsindikiza Sun uwanja wa ndege akisafiri kwenda nchini China lakini wakati wa ukaguzi alikamatwa akiwa na kiasi hicho cha fedha akikisafirisha bila kibali.
|
0 Comments