SHKUBAAli Khatibu Haji ‘Shkuba’.
Stori: Elvan Stambuli, UWAZI
DAR ES SALAAM: Ziko taarifa kwamba, wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya ‘unga’ nchini wamekuwa wakimiminika mkoani Lindi kwa lengo la kumnasua gerezani, mtuhumiwa wa biashara hiyo, Ali Khatibu Haji ‘Shkuba’ (45).

Kwa mujibu wa chanzo makini, wauza unga hao wamekuwa wakiweka vikao vya siri vya mara kwa mara jijini Dar es Salaam na Lindi lengo likiwa kuhakikisha mtuhimiwa huyo anatoka gerezani lakini bila kujulikana mbinu wanazotimia ili kufanikisha azma yao hiyo.
“Naamini mnajua kuwa, Shkuba bado yupo mahabusu ya Gereza la Mkoa wa Lindi kwa yale madai ya kuuza unga. Sasa nataka kuwaambia kwamba, wauza unga wenzake wamekuwa wakienda Lindi ili kumnasua jamaa.
“Kuna wakati wanafanya vikao hapa Dar, hasa maeneo ya Kinondoni mara nyingine kulekule Lindi. Lakini sijafahamu wanataka kumtoa kwa staili gani!
“Halafu pia, inawawia vigumu kufanikisha lengo kwa sababu wao wenyewe wengi wao ni vimeo, wanasakwa na jeshi la polisi,” kilisema chanzo hicho.
Minja 2Kamishna Minja.
Shkuba alinaswa saa sita usiku wa Februari 23, 2014 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar akijiandaa kwenda nchini Afrika Kusini na kuhusishwa na unga aina ya heroin kiasi cha kilo 211 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4 yaliyokamatwa Januari, mwaka jana mkoani Lindi.
Baada ya kukamatwa, alisafirishwa usiku huohuo kwenda Lindi chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo Februari 27, mwaka huo aliunganishwa na watuhumiwa wengine na kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kusini.
Watuhumiwa hao wengine ni pamoja na binti wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, Maureen Liyumba.
Shkuba ambaye ni mkazi wa Mikocheni, Dar ni mfanyabiashara mwenye maduka ya kubadili fedha (bureau de change) jijini Dar, pia ana makampuni ya ulinzi na anamiliki magari ya kifahari. Mali zake zote zilishikiliwa na serikali.
Wakati huohuo, Jeshi la Magereza Tanzania limesema kuwa, uwepo wa Shkuba kwenye Mahabusu ya Gereza la Mkoa wa Lindi umesababisha kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo hatoroki.
Mkuu wa Gereza la Lindi, Tusikile Mwaisabila alipopigiwa simu na gazeti hili alisema hawezi kuzungumza chochote kwa sababu msemaji wao ni kamishna jenerali wa magereza nchini.
mangu_eIGP Mangu.
Hata hivyo, Kamishna Jenerali John Minja,  wakati akielezea changamoto za magereza alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa za Kulevya jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita alizungumzia ulinzi uliopo Gereza la Lindi.
Aidha, alitoa wito kwa vyombo vinavyoshughulikia kesi ya mtuhumiwa huyo kuhakikisha upelelezi wake unakamilika haraka ili apelekwe mahakamani.
“Jeshi la Magereza limekuwa na changamoto ya uhaba wa fedha za kufanya ukarabati na upanuzi wa magereza ya zamani ili yawe na miundombinu inayoendana na ongezeko la wafungwa na mahabusu.
“Mfano mzuri unapokuwa na mtu kama Shkuba ambaye ni hatari hata kwa nchi kama Marekani, imetulazimu kuongeza  ulinzi katika Gereza la Lindi ambalo  yupo mahabusu mpaka sasa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa   Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu  alisema: ”Shkuba tulimkamata Februari, 2014 lakini alikana kuhusika licha ya waliokamatwa na unga kule Lindi kumtaja. Hivyo lazima tuchunguze ili kuthibitisha.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alipopigiwa simu juzi ili naye atoe maoni yake, iliita bila kupokelewa