Uchaguzi wa majimbo ya Afrika Kusini utafanyika Agosti tarehe 3 mwaka huu.
Rais Jacob Zuma alitangaza tarehe hiyo siku moja tu baada ya kuponyoka kura ya kutokuwa na imani naye bungeni iliyokuwa ikiongozwa na vyama vya upinzani kufuatia kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya mamlaka yake na mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini.

Rais Zuma anasema nia yake kuu ya kuitisha uchaguzi huo wa mashinani mapema ,ni kutathmini umaarufu wa chama chake cha ANC kufuatia tuhuma kuwa amepoteza uhalali wa kuiongoza taifa hususan baada ya kupatikana na hatia ya kupuuza maamuzi ya mahakama ya taifa hilo.
Zuma aliwataka wenyeji wajiandikishe kuwa wapiga kura kwa wingi iliwathibitishie upinzani kuwa kweli Afrika kusini imekomaa kidemokrasia.
Image captionViongozi wa makanisa pia wanamtaka rais Zuma ang'atuke madarakani
Wanaomkosoa wanasema ndie kiongozi asiye na umaarufu kwa wote tangu taifa hilo lijinyakulie uhuru wake mwaka wa 1994 na wanamtaka ajiuzulu.
Hii leo vyama vya kupigania haki za kibinadamu visivyo vya kiserikali vimejiunga na wale wanaomtaka ajiuzulu wadhfa wake vikisema amepoteza uhalali baada ya uamuzi huo wa mahakama ya juu.
Wengine waliomkaripia rais Zuma na kumtaka ajiuzulu ni aliyekuwa jaji wa mahakama ya juu Zac Yacoob, balozi mstaafu wa Afrika kusini nchini Uingereza Cheryl Carolus, kiongozi wa vyama vya wafanyikazi Zwelinzima Vavi kwa mujibu wa jarida la News24.
Image copyrightReuters
Image captionZuma amekiri makosa yake na amekubali kulipa fedha zote zilizotumika kufanyia ukarabati makaazi yake ya Nkandla.
Katika tukio la kushangaza, Tawi la chama tawala cha ANC cha jiji la Johannesburg, kimemtaka Zuma ajiuzulu.
Tawi hilo ndilo linalokabiliwa na ushindani mkubwa zaidi kutoka upinzani kwani wenyeji wake wamekuwa wakiwasikiza sana viongozi wa upinzani wakiongozwa na Julius Malema wa chama cha EFF.
Hata hivyo matawi mengine ya chama tawala ANC, ikiwemo lile la wanawake na pia la vijana yangali yanamuunga mkono rais Zuma.
Zuma amekiri makosa yake na amekubali kulipa fedha zote zilizotumika kufanyia ukarabati makaazi yake ya Nkandla.