Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei
DIWANI wa Kata ya Mtibwa, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lucas Edward Mwakambaya (38) mkazi wa Kidudwe wilayani Mvomero mkoa wa Morogoro, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kunajisi binti mwenye umri wa miaka 14.
Mtu huyo inadaiwa alikutwa Mei 29, mwaka huu saa 12 jioni akiwa katika nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Baraka iliyopo mtaa wa Sultan Area Manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema hayo jana ofisini kwake mjini hapa kwa waandishi wa habari, kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kukutwa na binti huyo alitiwa mbaroni.
Matei alisema, kukamatwa kwa diwani huyo, kulitokana na polisi kupatiwa taarifa kutoka kwa msiri mmoja ya kwamba katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Baraka iliyopo mtaa wa Sultan Area, kuna mtu mmoja ambaye alionekana na binti mwenye umri mdogo.
Hivyo alisema Polisi walifika katika nyumba hiyo ya wageni walifanikiwa kumkuta mtuhumiwa huyo akiwa na binti huyo ambaye jina lake limehifadhiwa katika chumba alichokodi namba 108 na hivyo kumtia mbaroni. Kamanda Matei alisema, binti huyo alitoka naye katika mji mdogo wa Turiani, ambapo pia mazingira aliyokutwa nayo yametiliwa shaka.
Pamoja na hayo, Kamanda Matei hakuweza kuelezea iwapo binti huyo bado ni mwanafunzi ama amemaliza elimu ya msingi. Kwa mujibu wa Kamanda Matei, hadi sasa mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Licha ya Kamanda wa Polisi kuzungumzia tukio hilo, mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Chadema Wilaya ya Mvomero, Mrisho Ramadhan , juu ya sakata hilo ambapo alikiri kuarifiwa kukamatwa kwa diwani huyo wa chama chake.
“ Ni kweli nimepata taarifa kuwa Diwani wa Chadema wa Kata ya Mtibwa, Lucas Mwakambaya amekamatwa na Polisi akiwa mjini Morogoro, lakini binafsi sijafahamu kosa alilofanya akakamatwa,” alisema Ramadhan. “ Nimewaomba viongozi wa Chadema mkoa wa Morogoro wafuatilie polisi ili kujua kilichomsibu diwani wetu na wanijulishe makosa yaliyosababisha akamatwe na polisi na kuwekwa ndani,” alisema Ramadhan.