Diwani wa Kata ya Mabatini Jijini Mwanza, Deus Mbehe (Chadema) akikata utepe kama ishara ya Uzinduzi wa Kikundi cha Kusaidiana cha USHIRIKIANO PEOPLE'S kinachoundwa na Wanachama zaidi wa 100 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Kata ya Mabatini.

Na BMG
Kikundi hicho kiliundwa baada ya kuibuka stofahamu ya wananchi kusaidiana katika masuala mbalimbali ikiwemo misiba, baada ya baadhi ya wanachama wa chadema kutengwa katika shughuli za misiba katika Kata ya Mabatini.

Uzinduzi wa Kikundi hicho ulifanyika katika Ukumbi wa Kilimanjaro uliopo Mabatini Stand huku ukiambatana na harambee kwa ajili ya kukiimarisha kikundi ambapo diwani wa Kata ya Mabatini ambae alimwakilisha diwani wa Kata ya Butimba, akichangia shilingi Laki Tano huku wageni wengine waalikwa wakifanikisha harambee hiyo kufikisha shilingi Milioni Moja, laki moja na elfu sabini.

Wanachama nao waliahidi kila mmoja kuchangia shilingi elfu kumi, pesa ambazo kwa ujumla zitasaidia kukabiliana na mapungufu yanayokikabili kikundi hicho. Mapungufu hayo ni pamoja na viti 120, sufuria nne, turubai mbili pamoja na sahani 200 lengo likiwa ni kujiimarisha katika mahitaji mbalimbali yanayohitajika katika shughuli mbalimbali.

Mwenyekiti wa Kikundi hicho chenye wanachama 103 hadi sasa, Salma Ibrahim, amewasihi wananchi wengine kujiunga na kikundi ili kuongeza nguvu ya kusaidiana katika masuala mbalimbali ikiwemo sherehe, misiba na kuinuana kiuchumi bila kujali itikadi zao za kisiasa.