|
SAKATA la ufichaji sukari lililoanzishwa na wafanyabiashara wasio waaminifu nchini, limechukua sura mpya baada ya Rais John Magufuli kutaja baadhi ya maeneo sukari hiyo ilikofichwa na kuagiza ikamatwe, itaifishwe na kugawiwa bure kwa wananchi.
Kwa sasa sukari imeshaanza kuadimika, ambapo katika maduka ambayo ilikuwa kawaida kukuta bidhaa hiyo katika makazi ya wananchi, haipatikani kabisa na inakopatikana, bei yake iko juu maradufu zaidi ya bei elekezi ya Sh 1,800 kwa kilo.
Takwimu za bei zimekuwa zikibadilikabadilika katika maeneo ya Dar es Salaam ambako wiki hii ilishafikia Sh 2,500 huku mikoani ikiongezeka na kuzidi Sh 3,000.
Walioficha Dar, Moro
Akizungumza jana na wananchi katika mji wa Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara akiwa njiani kwenda mkoani Arusha, Rais Magufuli alisema taarifa alizokuwa nazo mpaka jana kuna baadhi ya wafanyabiashara wameficha sukari tani 7,000.
“Kuna mmoja alienda kununua sukari Kilombero (mkoani Morogoro) zaidi ya tani 3,000 na kuiacha iko pale pale na mwingine ana godown (ghala) Mbagala (jijini Dar es Salaam), akiwa na tani 4,000 na hataki kuitoa ili wananchi wakose sukari, lakini nataka kuwaambia sukari huwezi kuficha kama sindano,” alisema huku akitoa mifano.
“Tutachukua sukari ile na kugawa bure na hawatafanya biashara maishani hapa nchini Tanzania, hivyo kama wapo wafanyabiashara wanaonisikia ambao wanataka kucheza na Serikali hii wanacheza na maisha yao,” alionya Rais Magufuli, ambaye uongozi wake umejivunia sifa ya kuchukua maamuzi ya kijasiri.
Kiwango hicho cha sukari iliyofichwa katika maghala mawili tu ya Morogoro na Dar es Salaam, kinatosheleza kulisha nchi nzima kwa wiki moja, kwa kuwa mahitaji ya siku ya sukari nchini ni tani 1,150 sawa na tani 420,000 kwa mwaka.
Salama la ambao hawajagundulika kwa mujibu wa Rais Magufuli, ni kutoa sukari waliyoficha kwa wananchi na kuiuza kadri walivyokuwa wamepanga. Kwa watakaokaidi, Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola kufuatilia wafanyabiasha wote walioficha sukari, kwani ni wahujumu uchumi na sukari waliyoficha itachukuliwa na kugawiwa bure.
Sababu ya kudhibiti
Akielezea sababu za kuzuia uagizaji wa sukari nje ya nchi, Rais Magufuli alisema wakulima nchini wanalima miwa, lakini haitengenezi sukari kwa kuwa kuna sukari ya magendo inayoingizwa kutoka nje ya nchi.
Mbali na kuwa ya magendo, Rais Magufuli alisema wafanyabiashara hao wanaoingiza sukari ya magendo, wana tabia ya ajabu kwenda nchini Brazil na maeneo mengine kunakouzwa sukari inayokaribia kuisha muda wake wa matumizi na kutaka kutupwa na kuinunua wao.
Alisema sukari hiyo ambayo katika nchi husika hutakiwa kumwagwa baharini, wafanyabiashara wenye tamaa ya fedha wa hapa nchini, huichukua na kuweka kwenye magunia tofauti na kuileta ndiyo maana wananchi wanapata magonjwa ya kila aina ambayo haijulikani yametoka wapi.
“Tunataka kudhibiti biashara hii ya sukari kwani tatizo ni dogo niwaambie ni la muda, kwani Serikali ya Magufuli haiwezi kushindwa kununua sukari hata kama ni mabehewa elfu ngapi,” alisema. Alisema ameshamuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na sukari ya kutosha italetwa na watu watapata bei ya sukari iliyo nafuu.
*Uagizaji kukomeshwa
Pamoja na uhaba uliopo ambao kwa sehemu kubwa umetengenezwa na wafanyabiashara hao baada ya kuzuiwa kuagiza sukari kutoka nje, tayari Serikali imeshachukua hatua za uzalishaji zaidi, zitakazokomesha kabisa biashara ya uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Wiki iliyopita wakati Waziri Mkuu Majaliwa akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni kuhusu pia bei ya sukari, alisema Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari kwa mwaka wakati mahitaji ya bidhaa hiyo kwa mwaka ni tani 420,000 na hivyo upungufu kuwa tani 120,000 kila mwaka.
Jana Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alielezea hatua hizo za kukomesha uagizaji wa sukari, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilango (CCM), aliyetaka kufahamu lini Mkoa wa Kigoma wenye rasilimali nyingi kutajengwa viwanda.
Kwa mujibu wa Mwijage, kiwanda kipya cha sukari kinatarajiwa kujengwa katika mkoa huo na tayari Serikali imeshampa mwekezaji wa kiwanda hicho, hekta za ardhi 47,000 kwa ajili ya mradi huo.
Mwijage alisema kiwanda hicho kitakapoanza uzalishaji, kitazalisha tani 120,000 za sukari kwa mwaka, ambazo ndizo zinazopungua katika uzalishaji wa sasa.
0 Comments