MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.
Anayetuhumiwa kuua mumewe Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.
Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.
“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.
Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.
‘Hausigeli’ asakwa Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.
Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.
Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.
“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.
Mamia wajitokeza msibani Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.
Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.
“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.
Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.
Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.
Gazeti hili pia lilifika Salasala, ambapo ndipo msiba ulipokuwa umeandaliwa na ndugu wa marehemu na kuhudhuria ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Salasala.
Ibada hiyo iliongozwa na Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Janeth Mwambungu ambaye alisisitiza waumini kwamba kifo ni mpango wa Mungu na kuwasihi kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.
“Tuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili tuache kumbukumbu ya maisha yetu, tuishi kwa faida… tukumbuke kwamba kufa ni faida na kila kifo ni mpango wa Mungu,” alisema.
Miongoni mwa waliohudhuria ibada ni wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango alikokuwa akifanya kazi Anathe.
Wasifu wa marehemu uliosomwa na Ofisa Tawala Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Geoffrey Mponda unaonesha Anathe alizaliwa Aprili 3, 1986 mkoani Arusha na alisoma na kuhitimu elimu ya sekondari kidato cha nne katika shule ya seminari Mt. Dorcus mwaka 2003.
Alimaliza kidato cha sita katika shule ya Lutheran Junior Seminari mwaka 2006 na kufaulu kwa daraja la kwanza na hatimaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2006/2007 na kuhitimu Shahada ya Uchumi mwaka 2009.
“Anathe hakuchoka kujiendeleza kusoma, Septemba 2009 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma Shahada ya Uzamili Uchumi (MA Economics) ambayo alihitimu mwaka 2011,” alisema.
Aliajiriwa Februari Mosi, 2012 kwa cheo cha Mchumi Daraja la II katika Wizara ya Fedha na Mipango. Alitembelea nchi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya kozi fupi zikiwemo Zambia, Rwanda, Kenya, Sweden, Marekani. Hadi mauti yanamfika alikuwa Mchumi Daraja la II katika Idara ya Uchambuzi wa Sera.
“Mbali na kuwa ni pigo kubwa kwa familia yake vile vile ameacha pengo kubwa katika Wizara ya Fedha na Mipango, hasa ukizingatia mchango wake ulikuwa bado unahitajika kwa wizara na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Mponda alisema Anathe alikuwa kipenzi cha wafanyakazi wenzake wote hasa kwa tabia yake ya ushiri