MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatarajia kuanzisha huduma mpya itakayojulikana kama “Mama na Mwana Afya Kadi” baada ya kupata mafanikio makubwa katika mradi wake wa majaribio katika mkoa wa Mbeya na Tanga.

Kuanzishwa kwa huduma hiyo kumeelezwa kuwa kutaboresha huduma za bima ya afya kwa kuyafikia makundi mbalimbali yenye mahitaji muhimu na adimu. Kwa uamuzi huo NHIF imepanua wigo kwa wanachama wa Mfuko huo ambao ni wachangiaji kwa kuangalia umuhimu wa makundi mbalimbali mojawapo ikiwa ni moja ya makundi yanayohitaji zaidi huduma za matibabu.
Uanzishwaji wa huduma kwa kundi hili ulielezwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Mfuko huo.
“Kuna makundi mengi ambayo yana mahitaji maalumu na yanauhitaji mkubwa sana katika eneo la huduma za matibabu, moja ya kundi ambalo sasa lazima tuanzishe huduma kwake ni hili la Mama na Mwana ili wawe na uhakika wa matibabu,” alisema Konga.
Alisema kuwa lengo kuu la huduma hiyo mpya ni kuwawezesha akinamama wajawazito na watoto kupata huduma za matibabu za uhakika ambazo Mfuko unatoa. Chimbuko la hatua ya huduma hii inatokana na matokeo mazuri na mafanikio makubwa ya mradi unaoendeshwa kati ya Mfuko wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) katika mikoa ya Tanga na Mbeya.
“Hatua ambayo imefikiwa kwa sasa ni kupata maoni ya wananchi kabla ya kuanza utelekezaji wake katika mwaka wa fedha wa 2016/2017,” alisema. Kutokana na hali hiyo, Kaimu Mkurugenzi huyo aliwataka watumishi wa Mfuko kuhakikisha wanajipanga kimkakati ili kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi kwa wanachama wanaojiunga na Mfuko kupitia makundi mbalimbali.
Alisema kuwa kwa sasa Mfuko umepanua zaidi wigo wake kwa wanachama ambapo matarajio ni Watanzania wengi zaidi kujiunga hivyo ni lazima watumishi na uongozi ujipange kukabiliana na changamoto zitazojitokeza lengo likiwa ni kutoa huduma bora kwa wanachama wake.
Hivi karibuni Mfuko pia umefanikiwa kuanzisha mpango mpya unaojulikana kwa jina la Afya Toto Kadi ambapo huduma hii imelenga kuwasaidia watoto wote chini ya umri wa miaka 18 ambapo mpaka sasa mwitikio ni mkubwa.