Maafisa nchini Burundi wanasema kwamba Rwanda imewafukuza zaidi ya raia elfu moja mia tatu wa Burundi kutoka nchini humo katika kipindi cha wiki moja iliyopita, baada ya wao kukataa kuhamishiwa hadi katika kambi ya wakimbizi.

Afisa mmoja amesema kuwa wale ambao walikataa kwenda katika kambi ya wakimbizi, walinyanganywa mali yao na kisha wakafukuzwa.
Makumi kwa maelfu ya Warundi walikimbilia Rwanda tangu ghasia zilipoanza nchini mwao mwaka mmoja uliopita, kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuwania Urais kwa muhula wa tatu kinyume na katiba.
Rwanda pia imewatimua Warundi ambao wameishi na kufanya kazi nchini humo kwa miaka mingi.