Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amesema Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete haikukomba fedha katika Hazina kama ambavyo baadhi ya wabunge wamedai, hata Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), lilifanya tathmini na kutoa taarifa safi.

Dk Mpango alieleza hayo bungeni jana mjini hapa, wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia mjadala wa wizara mbili zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Utawala Bora, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walisema Serikali ya Awamu ya Nne, ilikomba fedha zote Hazina na kusababisha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, kukuta Hazina haina fedha.
Akijibu hoja hiyo, alisema hakuna ushahidi ulioitia hatiani Serikali ya Awamu wa Nne kuhusu kukomba fedha Hazina na kwamba IMF na wadau wengine wa kimataifa, walifanya tathmini huru ya bajeti na mwenendo wa uchumi nchini na taarifa yao ya mwisho waliitoa Desemba mwaka 2015.
Katika ripoti hiyo hakuna mahali ilipoonesha nchi ilikuwa na hali mbaya ya fedha na kwamba kwa kudhihirisha hilo, vigezo vya kimataifa vilionesha bayana kuwa Deni la Taifa ni himilivu na nchi bado inakopesheka na imeendelea kulipa mishahara watumishi wake pamoja na madeni mengine bila kutetereka.
Alisema Serikali iliendelea kulipa madeni mengi na hakuna kilicholegalega, huku ikiendelea pia kugharimia shughuli za mihimili yote, ikiwemo Bunge, usalama wa nchi na kuendelea kulipa madai ya makandarasi na watoa huduma wengine.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imerithi mambo mengi mazuri yaliyofanywa na serikali za awamu zilizopita, ikiwemo uchumi imara, umeme uliosambazwa maeneo mengi vijijini na miundombinu.