Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

May 11, 2016

Serikali yaingiza sukari sokoni

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
SUKARI iliyoagizwa na serikali kutoka nje kwa ajili ya kujazia uhaba wa sukari kwa mfumo rasmi, imewasili nchini na tani takribani 12,000 zitaanza kusambazwa leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, alisema kuna upungufu wa sukari kwa mfumo rasmi, lakini serikali ilichukua hatua ya kuhakikisha inapatikana sukari kufidia uhaba huo na kuwa suala la sukari lisionekane kuwa tatizo kubwa.

“Sukari ipo lakini sio kwa kiwango halisi kinachopaswa kuwepo, lakini kama wafanyabiashara wangefanya biashara ya kuuza sukari kwa utaratibu mzuri uliowekwa wangekwenda sambamba na mfumo rasmi wa kuagiza sukari kujazia uhaba uliopo,” alisema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kiuhalisia zinahitajika tani 420,000 lakini uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha ni tani 320,000 kwa hiyo kuna upungufu wa tani 100000 na ndio maana serikali imelazimika kuagiza nje kufidia upungufu huo.
Alisema mkakati wa serikali ni kuimarisha viwanda vyake vya kuzalisha sukari, sambamba na kudhibiti sukari ya nje kuvifanya viwanda vya ndani vinakuwa na uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha pamoja na kuhamasisha wananchi kuwa na utamaduni wa kutumia bidhaa yao ya ndani.
Tani 11,957 zatua “Lakini tumechukua hatua kwa sasa kuagiza sukari nje tani 70,000 kujazia upungufu huo kwa sababu kwa sasa hivi viwanda vyetu havina uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha, vipo vingine vinahitaji kuboreshwa ama kukarabatiwa kabla havijaanza kazi,” alieleza Waziri Mkuu.
Alisema katika kujazia upungufu huo, tayari serikali imeingiza tani 11,957 ambazo zimeshawasili na zitaanza kusambazwa leo kikanda pamoja na kiwango cha tani kwenye mabano mikoa ya Kaskazini (tani 2,000), Kanda ya Ziwa (tani 3,000), Kusini (2,000), Nyanda za Juu Kusini (2,000) na Kanda ya Kati (2,000).
Alisema tani nyingine 24,000 za sukari, zinatarajiwa kuwasili Ijumaa hii na kwamba hadi kukamilisha taratibu na kutoka bandarini itakuwa kama Jumapili, hivyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu ijayo.
Waziri Mkuu alisema pia tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao na kwamba serikali inaamini upungufu uliokuwepo, utakuwa umejaziliziwa vizuri wakati ikitarajia ifikapo mwezi Julai viwanda vya ndani vitakuwa katika hali nzuri ya kuanza uzalishaji.
“Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani umesababishwa na watu wachache. Rais amekuwa makini kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na uhaba huo ikiwa ni pamoja na kuagiza waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe,” alisema.
Awabana wafanyabiashara Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara na wasambazaji wa sukari, watoe sukari na kuuzia wafanyabishara wadogo ili wao wauze kwa wananchi kwa bei elekezi ya Sh 1,800, sambamba na kuwataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kuhakikisha wanaendelea kusaka na kufichua watu walioficha sukari kwenye maghala yao.
Alisema serikali imeanza mkakati wa kuhakikisha uzalishaji wa sukari nchini unaongezeka kwa kuweka utaratibu mzuri wa namna wazalishaji wa ndani wanaweza kuzalisha katika viwanda vyao ili ifikapo mwaka 2019 tatizo la uhaba wa sukari liwe limemalizika.
Waziri Mkuu alisema mkakati mwingine wa serikali, kuboresha viwanda vya ndani na wamiliki wa viwanda pamoja na kualika wawekezaji kutoka nje ili waje kuwekeza hapa nchini kwenye viwanda vya sukari.
“Serikali ina maeneo matatu makubwa yako Bagamoyo, Ngerengere (Morogoro) na Kigoma, huku serikali ina mashamba makubwa ambapo mwekezaji atakayevutiwa anaweza kuja kupitia Kituo chetu cha Uwekezaji na kuona namna wanavyoweza kuwekeza katika sekta hii,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa kazi ya kufichua wafanyabiashara, wanaohodhi sukari nchini kwa nia ya kujinufaisha na kutaabisha Watanzania ni endelevu, lakini pia viwanda vya ndani vitakapoanza kuzalisha, serikali itaendelea kuhakikisha inadhibiti uingizaji wa sukari kutoke nje.
Dar yanasa tani nyingine
Mkoani Dar es Salaam, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, jana ilikamata sukari iliyokuwa imefichwa katika ghorofa moja lililopo wilaya ya Kinondoni eneo la Hananasif.
Sukari hiyo ambayo ni mifuko 160 yenye ujazo wa kilo 25, ilikamatwa baada ya kufanyika kwa msako katika nyumba hiyo inayomilikiwa na Bashiru Ismail baada ya kamati hiyo kupata taarifa kuhusu uwepo wa sukari hapo.
Mbali na kukamatwa kwa sukari hiyo katika Manispaa ya Kinondoni, pia kumebainika kuwepo sukari tani 52,000 zilizofichwa na mfanyabiashara ambaye anahangaika kuzificha. Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kushtukiza, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda alisema kukamatwa kwa sukari hiyo ni jitihada za kufuata agizo la Rais la kuwataka kuwafuatilia wafanyabiashara wanaoficha sukari na kusababisha wananchi wa hali ya chini kukosa bidhaa hiyo.
“Ni kosa kuhodhi bidhaa hii watu wasichukulie upungufu uliopo na kufanya wanayoyafanya wafanyabiashara wanatumia nguvu ili tuonekane hatuna uwezo wa kusambaza sukari,” alisema Makonda na kutoa mwito kwa wananchi kuwa sehemu ya kuwafichua wafanyabiashara wanaoficha sukari na kutoa taarifa kwa Dola.
Kwa upande wake, mmiliki wa jengo hilo, alisema sukari hiyo siyo ya biashara bali ni kwa ajili msaada ambao amekuwa akigawa kwa vituo vya watoto yatima waliopo katika vituo mbalimbali na watu wasiojiweza. Alisema ina miezi sita hapo na kwamba yupo tayari kuchunguzwa kama anauza.
Mbunge, Zakaria matatani tena
Nayo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi, wametoa saa 36 kwa Kampuni ya Al Naeem yenye sukari tani 1,840 zilizo bandarini, ziwe zimeingia sokoni na kuuzwa kwa bei elekezi.
Agizo hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru, Leonard Mtalay wakati taasisi hiyo na Jeshi la Polisi walipofanya ziara ya ghafla katika bandari ya Dar es Salaam ili kubaini ukweli wa taarifa za uwepo wa sukari iliyokaa muda mrefu bila kuingizwa sokoni.
“Tulipata taarifa kutoka kwa msiri wetu kuwa kuna sukari iko bandarini imehodhiwa na mfanyabiashara Turky (Salim Hassan- Mbunge wa Mpendae), ambaye hataki kuingiza sokoni na sisi kwa ushirikiano na Polisi tulifanya uchunguzi wetu na tulibaini ni kweli sukari hiyo ipo kontena 70,” alisema Mtalay.
Alisema katika uchunguzi wao, walimuuliza mfanyabiashara Turky kuhusu sukari hiyo na alikiri ni yake na katika uchunguzi wao walibaini pia kuwa sukari hiyo ilikuwa na mchakato mrefu wa kulipiwa kodi na kupata vibali.
“Tumebaini mengi, kuagiza sukari kunahitaji vibali na tumejiridhisha kuwa sukari hii imeshalipiwa kodi hivyo inatakiwa kuondolewa hapa na tumewapa Kampuni ya Al Naeem ambao ndio wanaonekana kuwa wamiliki wa sukari hii saa 36, kuanzia sasa, wawe wamefikisha sukari sokoni na kwa bei elekezi,” alisisitiza Mtalay.
Utata wa muda Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kampuni ya Al Naeem pamoja na Kitengo cha Huduma ya Makontena Bandarini (TICTS), kila mmoja alitoa taarifa inayokinzana na mwenzake kuhusu ukweli wa muda ambao sukari hiyo imefika bandarini hapo.
Kwa upande wa TRA, Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Jockton Kyamuhanga alisema sukari hiyo ina zaidi ya mwezi mmoja iko bandarini huku wamiliki wake wakifanya taratibu za kuitoa.
“Kampuni ya Al Naeem na patna wake Turky wanahusika na mzigo huo na taratibu za kutoa sukari hii zimechukua muda wa kama mwezi, vibali vyote vilikamilika tangu Ijumaa wiki iliyopita, sasa wanamalizia hatua za mwisho za kuiondoa bandarini,” alisema Kyamuhanga.
Alisema sukari hiyo haikuagizwa kutumika nchini, bali ilikuwa ipelekwe Bujumbura, Burundi na kwamba wahusika waliona hali ya siasa sio nzuri nchini humo na hivyo wakaiuza hapa nchini.
“Ni kweli sukari hii ilikuwa inapelekwa Burundi, ila mwenye mzigo alisema hali ya usalama na siasa nchini humo sio nzuri hivyo aliamua kuiuza kwa Al Naeem na huyo patna wake,” alisema Kyamuhanga.
Turky anena
Akizungumza na vyombo vya habari kwenye ukaguzi huo bandarini hapo, Turky alikana kuhusika na sukari hiyo na kusema yeye ni patna na mmiliki wa Kampuni ya Al Naeem, Haruni Zakaria.
“Mimi sihusiki na sukari hii, ila niko hapa kwa sababu mmiliki wa Kampuni ya Al Naeem ni patna wangu katika biashara, na nimekuja kumsaidia baada ya kusikia kuna vikwazo vya kutoa sukari, ila utaratibu umekamilika na sukari itatolewa na itakuwa sokoni,” alisema mbunge huyo wa CCM.
Aliongeza kuwa sukari hiyo ilikuwa inakwenda Burundi, lakini hali mbaya ya siasa nchini humo, imefanya sukari hiyo ibaki nchini na kutafutiwa vibali ili itolewe na kuuzwa hapa hapa nchini. “Ni miezi mitatu sasa sukari hii imefika hapa bandarini, ilikuwa sio ya hapa ilikuwa inaenda Burundi ila hali ya siasa sio nzuri na ndio tumeitafutia vibali ibaki nchini,” alidai Turky.
Meneja ya Al Naeem anena
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Al Naeem, Naeem Zakaria aliyekuwepo eneo la ukaguzi alisema wao walinunua sukari hiyo Februari mwaka huu na Machi mwaka huu, walilipia ushuru.
Aidha, kibali cha kuingiza sukari walikipata Mei 5, mwaka huu na vibali vingine vya ukaguzi wa ubora wa bidhaa hiyo kikiwemo kibali cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), walikipata Mei, 9 mwaka huu; hali inayozua maswali mengi kwa nini kama bidhaa hiyo haikupata vibali muda wote huo.
“Hizo zote hapa nilizo nazo ni vielelezo vya sukari hii, kampuni ilinunua sukari kutoka kwa kampuni ya India iliyokuwa ikipeleka sukari hii Burundi, sisi tumeinunua Februari mwaka huu, na Machi ndio tumelipia ushuru na Mei tukapata vibali, na jana Jumatatu (juzi) ndio tumepata kibali cha TBS,” alisema Zakaria.
Alisema kampuni hiyo ya India waliwafuata wenyewe ili wawauzie sukari hiyo kwa madai kuwa Burundi kuna machafuko hivyo hawawezi kuipeleka na kwamba baada ya kuinunua wamelipa kodi na tozo zote na sasa wanasubiri kuitoa sukari hiyo.
TICTS wanasemaje?
Kwa upande wao, TICTS walizungumzia muda sukari hiyo ilipoingia na kueleza kuwa ina miezi mitano tangu imeingia nchini na kwamba katika nakala za sukari hiyo zilionesha inakwenda Burundi.
Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa TICTS, Donald Talawa alisema wao walipokea sukari hiyo miezi mitano iliyopita na kwamba nakala za sukari hiyo iliyozalishwa Brazil, zinaonesha kwamba ilikuwa inakwenda Burundi.
“Sisi tulitoa kontena 70, ambazo 30 ziko hapa na nyingine 40 ziko bandari kavu yetu ya Ubungo, mara baada ya kuzipokea siku 21 zilipita bila mwenye mzigo kuutoa na sisi kama sheria inavyoelekeza tulikabidhi kontena hizo TRA,” alisema Talawa na kusisitiza kuwa kontena hizo zimekaa bandarini hapo bila kutolewa zaidi ya miezi mitano na sio mwezi mmoja na kwamba wao walishazikabidhi kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Agizo la Takukuru Akitoa agizo la sukari hiyo kuwa sokoni kuanzia leo, Mtakay alisema ni vyema wafanyabiashara wakatii maagizo ya serikali na kuacha tabia ya kuficha sukari, bali waitoe na kuuza kwa bei elekezi ya Sh 1,800, vinginevyo wakibainika bidhaa hiyo itataifishwa na kugawiwa kwa wananchi.
Habari hii imeandikwa na Angela Semaya, Sophia Mwambe na Ikunda Erick.
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP