Rais John Magufuli
JAMII ya Watanzania imetakiwa kujifunza sura za Rais John Magufuli, kutokana na hatua yake ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu hatua hiyo ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, alisema Rais ametuma salamu kwa sura nne kupitia utenguzi huo.
Sura ya kwanza kwa mujibu wa Minja, alisema Rais amewakumbusha watumishi wote wa umma kwamba uadilifu ni jambo muhimu mahali pa kazi, na wanapaswa kuheshimu na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia muda na sio kutumia muda huo vibaya.

Pili, Minja alisema Rais ametuma salamu kwa walio karibu yake, kwamba uswahiba wao hauhusiani na kazi ya nchi, hivyo suala la kufahamiana si kigezo cha kiongozi avunjaye maadili kuachwa, bali wanapaswa kutambua nchi inaongozwa kwa Sheria na Katiba.
Akizungumzia sura ya tatu ya uamuzi huo, Minja alisema Rais amewakumbusha Watanzania kuwa haangalii muda gani amemteua kiongozi au muda gani ametumikia nafasi aliyopewa, bali kinachoangaliwa ni utendaji kazi wake kwa Taifa.
Aidha sura ya nne, imeelezwa kwamba Rais ameoneshwa kuwa haendeshwi kwa siasa za vyama kwa kuangalia wanasiasa watasema nini, hasa wakati huu wa uwepo wa Sakata la Kampuni ya Lugumi, na kusema alichoangalia ni kosa limetendeka muda gani.
“Kwa kweli Rais kaonesha ukomavu wake, ameonesha ni Rais mwenye msimamo, bila kusita amefanya uamuzi sahihi, hakuangalia vyama vya siasa vinasema nini, bali aliangalia maadili ya utumishi wa umma yanasema nini na kuchukua hatua,” alisema Minja.
Watumishi wengine
Kwa upande wake Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa habari, Kitila Mkumbo, alisema uamuzi huo wa Rais ni hatua muhimu, na amefanya jambo kubwa na sahihi hivyo mawaziri wengine wanapaswa kuwa makini.
“Ni hatua kubwa, Rais amefanikiwa kuvuka hili, ameonesha uwezo wake wa kufanya uamuzi na sio kuangalia sura kwa minajili ya urafiki, au kufahamiana, ukiwa kiongozi unapaswa kujitambua hadhi yako na nafasi yako kwa jamii,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema hatua hiyo imesaidia Rais kuondokana na lawama ya Sakata la Kampuni ya Lugumi na inaashiria kwamba taasisi nyingine za Serikali zitafanya kazi zake mapema badala ya kumsubiri Rais afanye kila kitu.
Profesa Mkumbo alitoa mfano kwenye utenguzi huo na kusema Bunge lilikuwa na uwezo wa kumzuia asiingie ndani ya ukumbi ule kwa hali yake ya ulevi, ili asiiaibishe Serikali kama ambavyo imeonekana, lakini hawakuchukua hatua hadi Rais alipochukua.
“Sasa ni wazi kwamba Sheria za Kazi na Vileo maeneo ya kazi zitaanza kufanya kazi, ili kila mtumishi ajitambue na kufahamu wajibu aliopewa ni dhamana na anatakiwa kutekeleza kwa kuzingatia maadili,” alisema Profesa Mkumbo.
Jimboni nako watengue
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema Kitwanga ameachishwa kazi kwa fedheha na hata wapigakura wake kama sheria ingeruhusu wangemwajibisha.
Alisema cheo ni dhamana na kwamba katika nafasi aliyokuwa nayo ndani ya Baraza la Mawaziri tena kwenye wizara nyeti, alipaswa kuwa mfano wa kiongozi mwenye uadilifu na haiba yake ifanane na hicho chombo.
“Rais katuma salamu nzito kwa wengine na taasisi za umma, imetufundisha kuwa Rais akikupa wadhifa, usimuangushe, huyu kamuangusha Rais na Serikali, alipaswa kuwajibishwa na amewajibishwa kwa wakati, bila kushinikizwa,” alisema Dk Bana.
Alisema wananchi wanapaswa kumuelewa Rais na kuacha kuzungumza maneno yasiyo na maana kwani Kitwanga alipaswa kuwajibishwa kwa kosa alilotenda kwa wakati huo la ulevi na Rais amechukua hatua.
Dk Bana alisema kwa hatua hiyo ya Rais, ni wazi kwamba wale wote wenye wadhifa katika utumishi wa umma, wanapaswa kuheshimu na kuzingatia misingi ya Maadili ya Utumishi wa Umma na kama misingi hiyo huwezi kuitekeleza, ni bora waache kazi mwenyewe.
Misingi ya Nyerere
Kwa upande wake Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Dk Bashiru Ally, alizungumzia suala hilo kwa kurejea misingi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa katika mambo muhimu aliyoyajenga ni misingi ya utaifa na maadili ya utaifa.
Alisema kiongozi ni hadhi na ni nafasi ya heshima na kila kiongozi awe wa ngazi yoyote kuanzia Serikali za Mitaa hadi urais, anapaswa kutambua kuwa cheo ni dhamana na kina masharti na maadili yake.
“Ni mara ya kwanza kwa rais kuonesha ukali, ulevi ni jambo baya, linatakiwa kukemewa kwa nguvu zote, ujumbe huu uende kwa taasisi zote serikalini na kwa umma, pia walevi popote walipo hizi salamu ziwafikie,” alisema Dk Bushiru.
Alisema kosa alilofanya Kitwanga lipo kwa watumishi wengi wa umma na kwamba kwa hatua hizo za Rais, Katibu Mkuu Kiongozi anapaswa kupeleka salamu kwa taasisi zilizo chini yake kuwakumbusha kwamba utumishi wa umma unakwenda sambamba na maadili.
Swali kurudiwa
Kutoka bungeni, kitendo cha Kitwanga kujibu swali akiwa mlevi, kimesababisha Serikali kutakiwa kujibu upya swali hilo bungeni, huku akimkasirisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha, imefahamika kuwa watu wengi ‘walishitukia’ kuwa mbunge huyo wa Misungwi mkoani Mwanza hakuwa ‘sawasawa’ wakati akijibu swali bungeni Ijumaa asubuhi mjini hapa.
Uteuzi wa Kitwanga kwa wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi umetenguliwa na Rais John Magufuli juzi baada ya kubainika kuwa waziri huyo aliingia bungeni na kujibu swali linalohusu wizara yake akiwa amelewa.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa juzi kuhusu kutenguliwa uteuzi huo wa Kitwanga ilikuwa na aya mbili tu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20, Mei, 2016. “Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kufuatia kitendo cha Mheshimiwa Charles Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali linaloihusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa,” ilisema taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Hali ilivyokuwa
Awali asubuhi, Kitwanga akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema) ambalo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema). Katika swali la nyongeza, Kiwanga alihoji Wilaya ya Kilombero ina miaka 55 lakini polisi hawana nyumba wamepanga na Jimbo la Mlimba wanaishi kwenye nyumba za Tazara, hivyo serikali ipewe miaka mingapi kujenga nyumba na vituo vya polisi.
Kitwanga alijibu: “Kwani wewe una miaka mingapi? Usiulize miaka ya kujenga nyumba za Polisi na vituo. Amini tutajenga tu. Halafu wewe ni rafiki yangu lazima nikujibu hivyo.” Hata hivyo, majibu hayo na jinsi alivyokuwa akijibu, yaliwashitua wengi wakiwamo waandishi wa habari ambao hawakumwelewa vizuri Kitwanga. “Hivi mbona Kitwanga leo yuko hivi? Yuko sawa sawa kweli,” alihoji mwandishi mmoja wa habari.
Hata wakati wa jioni kabla ya baadaye kutangazwa taarifa za kutenguliwa kwa wadhifa wa Kitwanga, mwandishi mwingine ambaye hakuwamo ndani ya ukumbi wakati Kitwanga anajibu maswali, aliuza: “Jamani hivi asubuhi wakati Kitwanga anajibu maswali alikuwaje.”
Alijibiwa na wenzake kwamba hakuonekana kuwa sawasawa, na mwingine akaenda mbali zaidi na kueleza kwa alionekana amelewa. Waziri huyo alitembelewa na wapigakura wake kutoka jimboni na walitambulishwa miongoni mwa wageni waliofika bungeni juzi.
Kuitwa na Waziri Mkuu
Lakini baada ya hali hiyo kutokea, inaelezwa kuwa baada ya kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni, Kitwanga aliitwa ofisini kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye awali alikuwamo bungeni.
Inaelezwa Waziri Mkuu alikuwa amekasirika sana kutokana na kilichofanywa na waziri huyo na hakuwa yule aliyezoeleka miongoni mwa watu wake.
Kilichoendelea kati yao hakikufahamika, lakini kuna kila dalili alizungumza na Dk Magufuli kutokana na kitendo cha uvunjifu wa maadili ya utumishi kilichofanywa na Kitwanga, na kusababisha rais kutengua uteuzi wake.
Katika taarifa yake juzi usiku saa chache baada ya kutimuliwa Kitwanga, Waziri Mkuu Majaliwa alisema uamuzi uliofanywa na Dk Magufuli umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao unakataza mtumishi kulewa akiwa kazini.
“Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi hatakiwi kunywa pombe na wala hapaswi kulewa akiwa kazini… mtumishi anapaswa kuwa na akili timamu inamwezesha kufanya kazi za Serikali,” alisema Majaliwa akijibu swali la mwandishi wa TBC1 aliyetaka kujua ukweli wa taarifa za kutimuliwa Kitwanga. “Ni kweli Mheshimiwa Rais, Dk John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei, 2016 baada ya kuonekana amelewa wakati wa kazi. Na hili lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake leo asubuhi,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, kutokana na majibu ya Kitwanga kutoridhisha, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) aliomba mwongozo wa Spika kwamba swali la Minja halikujibiwa kwa ukamilifu.
Kwa kawaida, maswali bungeni hujibiwa na naibu mawaziri kwa kila wizara, na endapo wizara haina naibu, hujibiwa na waziri husika. Na endapo wote hawapo, huteuliwa naibu waziri mwingine kujibu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni hakuwapo bungeni juzi na imefahamika kuwa yuko safarini kikazi katika moja ya mikoa nchini. Kwa mujibu wa Naibu Spika Dk Tulia Ackson, swali la Minja lilikuwa: “Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi, ikilinganishwa na kazi zao wanazozifanya kwa jamii? Je, serikali ina mpango gani wa kuwaboreshe askari makazi.”
Akitoa majibu ya mwongozo huo juzi usiku kabla ya kuahirisha Bunge, Dk Ackson alisema ilibainika kuwa si kwamba swali la Minja halikujibiwa kikamilifu na Waziri, ila majibu yake hayakutoa mchanganuo wa nyumba ngapi zitajengwa kwa upande wa askari wa Jeshi la Magereza.
“Kwa kuzingatia Mwongozo ulioombwa na Mheshimiwa Mbunge, na uzito wa swali lililoulizwa kiti kimeamua kuelekeza swali hilo lirudiwe kuulizwa katika kikao cha tarehe 23 Mei, 2016. “Ili serikali iweze kutoa majibu kwa ufasaha zaidi ikiwa ni pamoja na kutoa mchanganuo wa nyumba ngapi za Askari Magereza zitajengwa, na katika maeneo gani,” alisema Naibu Spika.
Kitwanga aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Nishati na Madini anakuwa waziri wa kwanza kutimuliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Mapema wiki hii, akifanya majumuisho ya hotuba yake ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema yeye anatambulika kwa jina la ‘Bwana STK.’ “Niko serikalini kwa miaka 35 sasa. Natambulika kama Mr STK, Mzee wa STK – Sheria, Taratibu na Kanuni.
Nimewasilisha fomu yangu Sekretarieti ya Maadili kwa mara ya kwanza mwaka 1998. “Hivyo vinatosha kuwapa taarifa mimi ni mtu wa aina gani, sipendi kusema, napenda kutenda,” alisema Kitwanga ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Dk Magufuli.
Imeandikwa na Mgaya Kingoba, Dodoma na Ikunda Erick, Dar.