RIADHA Tanzania (RT) ina safari ndefu kurejea katika mafanikio ya miaka ya 1970 hadi 1990 wakati wanariadha wake walipotamba duniani kwa kufanya vizuri katika mchezo huo.
Huko nyuma wanariadha wa Tanzania kama akina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa, Francis Naali, Simon Mrashani, Gerway Suja, Samson Ramadhani, Gidamis Shahanga na wengine wengi walifanya maajabu duniani. Hata hivyo, miaka ilivyokwenda wanariadha wa Tanzania wameshindwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali na kufanya kukosa mialiko ya kushiriki mbio kubwa kama zile za London Marathon, New York, Boston, Lake Biwayo na zingine.

Sababu kubwa ya wanariadha wa Tanzania kukosa mialiko hiyo ni kwa sababu ya kutofanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Wanariadha wanapofanya vizuri katika mashindano au mbio za mialiko na zile za Olimpiki, Jumuiya ya Madola na hata za Afrika, mawakala au waandaaji wa mbio wamekuwa wakiwapa mialiko ili kuweka ushindani katika mbio zao kwa kuwa na wanariadha nyota.
Mashindano ya U20
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha ya Afrika Mashariki na Kati kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 29 na 30. Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya nchi 10, ambazo ni wenyeji Tanzania Bara, Zanzibar, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Uganda na Sudan Kusini. Timu ya Tanzania ilipiga kambi katika hosteli za Filbert Bayi zilizopo Mkuza Kibaha mkoani Pwani chini ya makocha Robert Kalhahe na Mwinga Mwanjala.
Timu hiyo ilikaa kambini kwa wiki mbili, lakini ilichelewa kuanza kambi kutokana na ukata licha ya RT kuahidi kuweka timu hiyo kambini mapema. Mashindano hayo yalifanyika vizuri, lakini changamoto zilikuwa nyingi ikiwemo watazamaji wachache pamoja na timu yetu kutofanya vizuri.
Watazamaji wachache
Tofauti na ukubwa wa mashindano hayo, lakini watazamaji walikuwa wachache na hiyo ilitokana na Riadha Tanzania (RT) kutoyatangaza vizuri mashindano hayo. Pia, RT walitakiwa kupiga hodi katika shule mbalimbali za msingi na sekondari za jijini Dar es Salaam na kuwashawishi walimu wa shule hizo kuwaruhusu wanafunzi wao kwenda kushuhudia mashindano hayo.
RT walitakiwa hata kugharamia usafiri wa wanafunzi hao kwenda Uwanja wa Taifa na kuwarudisha shuleni kwani mashindanohayo yanapomalizika hiyo ingesidia wanafunzi wengi kujitokeza na kuwashangilia wenzao. Mchezo huo hapa nchini hauna wapenzi wengi kwa sababu ya kutofanya vizuri, lakini kama tungekuwa tunafanya vizuri kimataifa bila shaka tungekuwa na mashabiki wengi kama nchi za Kenya, Ethiopia na hata Uganda.
Kuvurunda katika mashindano Wenyeji Tanzania Bara walishindwa kufurukuta licha ya makocha na viongozi wa RT kutamba kuwa timu hiyo imejiandaa vizuri na itawika katika mashindano hayo. Timu hiyo ilishika nafasi ya sita kati ya timu 10 zilizoshiriki huku ikiambulia medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na saba za shaba.
Ukweli unabaki pale pale kuwa wenyeji hawakufanya vizuri kwani walistahili kumaliza ndani ya tatu bora. Wenzetu Zanzibar wenyewe walimaliza katika nafasi ya tano baada ya kupata medali mbili za dhahabu, moja ya fedha na nne za shaba na kuondoka na jumla ya medali saba sawa na Tanzania Bara. Kufanya vibaya kwa Tanzania Bara ni muendelezo wa timu zetu kuvurunda katika michezo mbalimbali kwa miaka mingi sasa.
Changamoto zingine
Mbali na kuambulia nafasi ya sita huku majirani zetu wa Kenya na Uganda wakimaliza katika nafasi ya kwanza na pili, wanariadha wetu hawakuwa na mbinu za kimashindano. Wanariadha wetu walijitahidi kuanza kwa nguvu na kuongoza, lakini walishindwa kumaliza vizuri na kujikuta wengi wao wakiwa nje ya tatu bora na hivyo kukosa medali yoyote.
Wenyeji walikuwa wa jumla ya wachezaji 27 wakiwa ni wengi zaidi ya nchi zingine, lakini walishindwa kutumia vizuri wingi wao huo na kujikuta wakimaliza mbio nyuma ya wenzao. Riadha ni staili ya ukimbiaji lakini wanariadha wetu karibu wote walikuwa hawajui jinsi ya kukimbia kwani wengine walishindwa hata kurusha mikono vizuri na hata jinsi ya kukimbia.
Tatizo kubwa linaonekana liko katika msingi wa wanariadha wetu, kwani kuna mbinu walitakiwa kufundishwa tangu utotoni na sio kusubiri wanapoitwa katika timu ya taifa ndio waanze kufundishwa jinsi ya kukimbia na kutafuta pumzi. Makocha wa timu za taifa za riadha jukumu lao kubwa ni kuwapa baadhi ya mbinu wanariadha na sio kuwafundisha hatua ya mwanzo kabisa ya kukimbia, hilo ni tatizo kubwa.
Wasemavyo makocha, wanariadha?
Kalyahe anasema kuwa sababu kubwa ya kufanya vibaya ni maandalizi ya muda mfupi, hasa ukizingatia kuwa wachezaji wengi hawakuwa na mazoezi ya kutosha huko walikotoka. Anasema mashindano yalikuwa magumu na wachezaji wake walijifunza kitu kutoka katika mashindano hayo hasa umakini wa mchezaji kuwa fiti wakati wote kwa ajili ya mashindano husika.
Anaiomba Serikali kurudisha mfumo wazamani, ambapo majeshi yalikuwa yakiandaa wachezaji hasa riadha kwa muda mrefu na pamoja na kuajiriwa, lakini shughuli zao kubwa zilikuwa ni mazoezi tu asubuhi na jioni. Anasema kuwa timu ya taifa sio mahali pakujifunzia kwani wachezaji wanapata mafunzo ya awali katika klabu zao na katika timu ya taifa wanapata mafunzo ya muda mfupi tu.
Filbert Bayi
Bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za meta 1,500 na mshindi wa medali ya fedha wa Michezo ya Olimpiki kwa meta 3,000 kuruka maji na gogo, Filbert Bayi anasema kuwa tatizo la kufanya vibaya ni ukosefu wa makocha wenye uwezo wa kufundisha. Bayi ambaye pia ni bingwa wazamani wa dunia wa maili moja anasema kuwa mbali na makocha kuwa na uwezo mdogo, pia wamekuwa wakitumia muda mwingi kupiga domo badala ya kufanyakazi.
Dk Hamad Ndee
Makamu wa Pili wa Rais wa Riadha Tanzania (RT) upande wa Ufundi, Dk Hamad Ndee anasema kuwa bila ya Serikali kuwekeza katika michezo kamwe hatuwezi kufanya vizuri. Anasema kuwa nchi zote ambazo zimefanya vizuri katika mashindano hayo na mengine, serikali zao zimewekeza katika michezo na hasa riadha. Anasema kuwa kama hatutawekeza kamwe tusitarajie miujiza kufanya vizuri katika mashindano makubwa kwani wanariadha wetu hawako vizuri kwa ushindi.
Dk Mdee ambaye pia ni mhadhiri wa Elimu kwa Michezo kupitia shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni mwanzilishi wa kozi hiyo mwaka 1993 na ni chuo kikuu pekee nchini kinachotoa shahada ya elimu ya michezo. Pia Dk Mdee wakati wa uchezaji wake alikuwa mkimbiaji wa mbio za meta 100, 200 na 400 na kuliwakailisha taifa katika michezo mbalimbali ikiwemo ile ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na All African Games katika miaka ya 1970 na kuendelea.
Kingine kikubwa hakuna ofisa michezo yeyote aliyepitia UDSM ambaye hajapita mikononi mwake. Alitolea mfano Tanzania ilipokuwa ikifanya vizuri huko nyuma, ambapo wanariadha kama akina Bayi walipokuwa waking’ara alisema wakati huo serikali iliwekeza katika michezo na hasa riadha.
Anasema kuwa michezo ilisaidia sana kuitangaza vizuri Tanzania mfano Bayi alipoweka rekodi ya dunia ya mbio za meta 1,500 katika Michezo ya Jumuya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand mwaka 1974, “dunia nzima ilitaka kuijua Tanzania iko wapi?”Anasema kuwa Tanzania inaweza kufanya vizuri kimataifa kwani ina wachezaji wazuri na wenye vipaji vya hali ya juu, lakini wanachokosa ni uwekezaji tu ndio haupo.
Francis John
Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania inayojiandaa kwa ajili ya kushiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki itakayofanyika Rio, Brazil Agosti mwaka huu, Francis John anasema maandalizi yalikuwa hafifu sana. Anasema timu yetu tangu mwanzo ilionekana ni dhaifu sana na ili kufanya vizuri katika mashindano yajayo, “tunatakiwa kuwaandaa mapema wanariadha wetu tena kwa muda mrefu.”
Alisema kambi za muda mrefu pia zinahitaji fedha nyingi, hivyo RT wanatakiwa kushirikiana na serikali kufanikisha hilo. Naye bingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20, Gulam Khamisi anasema kuwa mashindano yalikuwa mazuri na walikwenda kutekeleza ahadi waliyoitoa kwa Rais wao Dk Ali Mohamed Shein. “Tulimuahidi rais ushindi na tumekuja kutekeleza kile tulichokiahidi cha kurudi na medali,” anasema Khamisi.
Mashindano yenyewe
Kiujumla mashindano hayo ya wachezaji chini ya umri wa miaka 20 yaliendeshwa kitaalamu kwa usimamizi wa Wachina, ambao walijenga uwanja huo, kwa ajili ya matumizi ya vifaa vya riadha, ambavyo vilitumika katika mashindano hayo.
Baadhi ya vifaa vilivyotumika ni pamoja na kamera (photo finishing), ambazo hutumika kumpata mshindi endapo wanariadha zaidi ya mmoja watamaliza pamoja katika mbio na kwa mtazamamo wa kawaida huwezi kumpata mshindi. Vifaa vingine ni vile vya kuonesha muda, vifaa vya kuanzia mbio hasa zile fupi (starting blocks) na vingine kama screen kubwa ambalo lilikuwa likionesha muda na ratiba za kila mbio.
Waliopata medali Wanariadha wa timu ya Tanzania Bara waliopata medali ni pamoja na Sabas Daniel aliyepata medali katika mchezo wa kurusha kisahani na ule wa mkuki na Mwanahamina Hassan aliyepata medali katika kutupa mkuki kwa wanawake.