Mnadhimu wa Bunge wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu
WABUNGE wanawake kutoka Kambi ya Upinzani inayoundwa na vyama vilivyoko katika kundi la Ukawa, jana walitoka nje ya Bunge baada ya kukerwa na neno ‘bebi’, lililotumiwa juzi na Mbunge wa Ulanga Mashariki Goodluck Mlinga (CCM).
Mlinga alichafua hali ya hewa ndani ya Bunge juzi jioni, wakati akichangia katika Ba ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, baada ya kusema wanawake waliopata ubunge kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepata nafasi hiyo baada ya kuitwa ‘bebi’.

“Kila mwanamke ndani ya Chadema kaingia ubunge kwa sifa yake lakini sifa kubwa ni lazima uitwe bebi. Chadema kuna wanachama wengi wa kike iweje ichukue wa CCM. Chadema ndiyo inakandamiza demokrasia, Tundu Lissu anajua sheria lakini ndani ya Chadema kuna wapenzi wa jinsia moja,” alisema.
Baada ya kutoa kauli hiyo majira ya saa 11:39 jioni, hali ilibadilika ndani ya Bunge, walisimama wabunge wote wa Chadema na CUF wakiomba utaratibu na kupiga kelele za kuonesha kukerwa na kauli hiyo.
Waliendelea kupiga kelele licha ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwataka watulie na hali hiyo iliendelea kwa takriban dakika nne na kumfanya Naibu Spika kumuomba Mnadhimu wa Bunge wa Kambi ya Upinzani, Lissu awatulize upande wa upinzani.
“Naomba mtulie, naomba mtulie, Lissu watulize watu wako ili tuendelee,”alisema na baada ya sekunde chache wabunge wote walikaa chini na Lissu akasimama na kuzungumza.
Kauli ya Lissu
Lissu alisema “Kanuni ya 64 inakataza mbunge kumsema vibaya mbunge mwingine au kumdhalilisha mtu mwingine, mjumbe aliyemaliza kuzungumza (Mlinga) katoa maneno ya udhalilishaji kwa wanawake na kukiuka kanuni za Bunge. “Kama msemaji anabisha hoja basi abishie hoja lakini amesema mambo ya nje ya Bunge, amezungumzia mahusiano binafsi, naomba kiti chako kichukue hatua stahiki ili lugha ya kudhalilisha wanawake ikome,” alisema Lissu.
Naibu Spika Baada ya Lissu kumaliza, alisimama Naibu Spika na kusema “Lissu ametukumbusha mambo yasiyoruhusiwa, lugha zinazotumika humu pande zote mbili haziko sahihi, tutumie lugha za kibunge, kuita wengine wajinga au tabia za watu fulani hazifai. Goodluck endelea kwa lugha nzuri”.
Hata hivyo Goodluck alishindwa kuendelea licha ya kupewa nafasi kutokana na wabunge wa upinzani kusimama na kupiga kelele wakimtaka afute kauli yake.
Kitendo hicho kilimfanya tena Naibu Spika kusimama na kuwataka wakae chini kisha akampa nafasi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
*Mhagama
Mhagama alisema; “alichosema Naibu Spika ni sawa, pande zote mbili kumetolewa lugha zisizofaa, sisi mawaziri tumetukanwa tukiambiwa wajinga, kuna mtu kaitwa kigodoro humu, si haki kuruhusu upande mmoja utukanwe, Naibu Spika tumia kiti kufuta maneno yote ya matusi ya leo,” alisema.
Naibu Spika akasema “naagiza maneno ya udhalilishaji kwa CCM na upinzani yafutwe,” ndipo akaruhusiwa Goodluck kuendelea naye akafuta kauli yake.
Waamka nayo
Jana Mbunge wa Viti Maalumu Sophia Mwakagenda (Chadema), aliomba mwongozo wa Spika kutokana na kauli ya juzi ya Mlinga na aliporuhusiwa, alisema kauli hiyo ni ya udhalilishaji si kwa wabunge wanawake wa upinzani, bali kwa wanasiasa wote wanawake na haipaswi kupigiwa makofi.
“Hata Rais wetu aliyepita (Jakaya Kikwete) alitambua umuhimu wa kutoa nafasi kwa wanawake na ndio maana uteuzi wake ulizingatia usawa. “Sasa imenishangaza hapa bungeni pamoja na mbunge huyu kutoa kauli za udhalilishaji dhidi ya wanawake, wapo wanawake wenzetu wanashangilia na tena na kupiga makofi,” alisema Mwakagenda.
Alisema akiwa mwanamke mwanasiasa hataki kuamini kama wanawake wote waliomo ndani ya siasa, wamepitia kwanza kwenye mchakato wa uzinifu ndipo wakafanikiwa kupata nafasi za uongozi.
Alisema kutokana na kitendo cha Chama cha Wanawake Wabunge kutochukua hatua zozote dhidi ya kauli hiyo iliyodhalilisha wanawake, anajivua rasmi uanachama wa chama hicho.
Dk Ackson wakati akijibu mwongozo huo, alisema tayari alishatolea mwongozo kauli hiyo tangu katika mjadala wa juzi jioni wa kupitisha makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Katiba na Sheria.
“Nilisema kuwa pande zote mbili zilitumia maneno mabaya na kuagiza kauli hizo zifutwe kwenye taarifa za Bunge. Kwa maana hiyo naomba tuendelee na ratiba,” alisema Naibu Spika.
Vurugu
Baada ya kauli yake hiyo wabunge hao wanawake wa upinzani hawakukubali, wakaamua kusimama huku wengi wao wakiomba taarifa na miongozo ingawa hawakupatiwa nafasi.
Mara baada ya Dk Ackson kumaliza kutambulisha wageni waliofika bungeni hapo, vurugu ziliibuka tena bungeni hapo, ambapo wanawake wote wa upinzani walisimama huku wakipinga Bunge kuendelea bila mwongozo huo kujibiwa.
“Nawaomba mkae, suala hili silizungumzii tena nimeshalipatia majibu. Waheshimiwa kaeni chini, nasema kaeni chini,” alisema Naibu Spika kauli ambayo hata hivyo wabunge hao hawakuitii.
Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea bungeni hapo, baadhi ya wabunge wa upinzani walisikika wakirusha maneno ya kejeli dhidi ya Naibu Spika huku wakidai kuwa wao si wanafunzi na kiongozi huyo wa Bunge si mkuu wa shule.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alisikika akisema; “msituburuze, usitumie kiti vibaya tuna haki kwa mujibu wa sheria, tunaomba kupewa nafasi ya mwongozo hatuwezi kuvumilia udhalilishaji huu.”
Dk Ackson aliyekuwa pia amesimama aliwafokea wabunge hao kwa kuvunja kanuni inayowataka wakae chini wakati yeye amesimama. “Waheshimiwa kaeni chini, nasema mliosimama kaeni chini, nimesema kaeni chini, ninawaomba kwa mara ya kwanza jamani kaeni chini tuendelee.”
Watolewa nje
Baada ya jaribio la kuendelea na ratiba kushindikana kutokana na kelele za wabunge hao, Dk Ackson alilazimika kuwaagiza wabunge hao watoke nje, agizo ambalo walijaribu kukaidi hadi pale askari wa Bunge takriban watatu walipowasili.
Wakati wakiondoka ndani ya Bunge hilo, wabunge hao akiwemo Mdee na Esther Bulaya (Chadema), pamoja na baadhi ya wabunge wa upinzani walitupa hewani vitabu vya Bunge vilivyokuwa kwenye meza zao za shughuli za Bunge kwa siku hiyo.
Baada ya wabunge hao kutoka nje huku wakifuatwa nyuma na mbunge wa Urambo Mashariki ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho cha TPWG Margaret Sitta, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), aliendelea kuomba mwongozo lakini Dk Ackson alimkatalia.
“Acha kutuburuza bwana,” alisema Msigwa huku akiwa amekasirika na kuchukua vifaa vyake na kutoka nje. Wakiwa nje wa ukumbi wa Bunge, Mdee aliyezungumza kwa niaba ya wabunge wenzake wanawake wa Ukawa, alisema Naibu Spika amevunja Katiba kwa kukataa kuwaruhusu watoe miongozo yao kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.