|
SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kutaja idadi ya watumishi hewa kuwa ni 7,200, msako unaoendelea katika utumishi wa umma, umetoa takwimu mpya ambapo sasa watumishi hao wamefikia 8,236.
Katika hatua nyingine, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ambao wamefunguliwa kesi mahakamani kutokana na ubadhirifu, ambao wamekuwa wanatumia magari na mafuta ya umma na kujilipa posho wanapokwenda kwenye kesi zao, wataanza kuchukuliwa hatua kali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema hayo bungeni jana wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha.
Akizungumzia wafanyakazi hewa, Waziri Kairuki alisema kati ya Machi Mosi na Aprili 24, mwaka huu, Serikali imebaini kuwepo kwa watumishi hewa 8,236, idadi inayoonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa baada ya hivi karibuni Rais kuripoti kuwepo wafanyakazi hewa 7,200.
Alisema katika idadi hiyo, wafanyakazi hewa 1,614 wameripotiwa kutoka Serikali Kuu huku wengine 6,622 wakiripotiwa kutoka Serikali za Mitaa, na kufanya ongezeko lao kufikia 2,737.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, kuwepo kwa wafanyakazi hao hewa katika utumishi wa umma kumeisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 15.4, ambazo zingeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema katika kushughulikia hilo, Serikali imelazimika kuwasimamisha kazi maofisa utumishi 56 ambao walibainika kuhusika kufanikisha malipo ya mishahara kwa watumishi hao hewa na hatua mbalimbali za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
‘’Hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao na endapo watabainika kuwa na makosa kisheria, watalazimika kurejesha fedha za Serikali zilizopotea kutokana na malipo hayo hewa ya mishahara,” alisema Kairuki.
Kuhusu wakurugenzi wa halmashauri wenye kesi za ubadhirifu mahakamani, Waziri Kairuki alisema Serikali inafanya uchunguzi kuhusu wakurugenzi hao ambao kutokana na kuwa na kesi mahakamani, wanatumia fedha na rasilimali za Serikali kwenda kuhudhuria kesi zao.
“Zipo taarifa hizo kwamba wakurugenzi hawa wanakwenda katika kesi hizo wakiwa wamejilipa posho za kujikimu za Serikali wao na madereva wao lakini pia wakitumia magari na mafuta ya Serikali. Ikibainika kuwa wapo wakurugenzi kama hawa hatua kali zitachukuliwa kwao mara moja,” alisema Waziri Kairuki.
0 Comments