Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
UJENZI wa Mradi wa Kusindika Gesi (LNG) mkoani Lindi utakaowezesha nchi kuanza kufanya biashara ya gesi nje ya nchi umeanza baada ya jana wadau sita wa mradi huo kukutana na kupeana elimu kabla ya mchakato mzima kuanza wakati wowote mwaka huu.

Kwa kutumia mradi huo, Tanzania itaanza kufanya biashara ya gesi kwa kuuza nje ya nchi baada ya kubaini kuwa gesi iliyogundulika baharini inayofikia kiasi cha futi za ujazo trilioni 47, ni nyingi na ikivunwa mahitaji ya ndani hayawezi kuimaliza hivyo kulazimika kuiuza nje ya nchi na kuongezea Taifa mapato.
Akizungumza jana katika mkutano wa wawekezaji na serikali kupata elimu ya mradi huo kabla ya kuundwa kwa kamati ya majadiliano ya serikali na kuingia mkataba wa ujenzi, Mkurugenzi wa Utafiti wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kelvin Komba alisema wamekutanisha wadau kutoka serikalini na wawekezaji.
Komba alisema mkutano huo ni kuanza taratibu za awali kuwekeza na kuuza gesi kwa kutolewa kitaalamu rasilimali hiyo kwenye visima na kufikishwa katika mtambo huo wa LNG ambao utaigeuza kuwa kimiminika ili ifae kuingizwa katika matangi na kusafirishwa kwa meli kwenda katika masoko mbalimbali duniani.
Akifafanua zaidi, alisema mtambo huo utaipooza gesi itakayovunwa mpaka nyuzi joto sifuri na kuipooza zaidi mpaka nyuzi joto hasi 100, ndipo inakuwa kimiminika na kufaa kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali duniani.
Mradi huo mkubwa ambao haujawahi kutokea katika historia wa miradi nchini wenye thamani ya inayofikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 60 na kutoa ajira karibu 20,000, utawezesha nchi kukua kiuchumi.
Alisema tayari ardhi imepatikana ya hekta 2,071 kwa ajili ya mradi wa LNG huku hekta nyingine 20,000 zinazozunguka eneo la mradi huo, zikitengwa kwa ajili ya viwanda. Alizitaja kampuni sita zinazoshirikiana katika ujenzi wa mtambo huo ni TPDC, BG Group, Ophir Energy, Statoil, Exxon Mobil na Pavilion Energy. Mradi huo thamani yake ni kuanzia Dola za Marekani bilioni 30 mpaka bilioni 60.