Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kusikitishwa na tukio la mauaji ya watu saba wa familia moja waliokatwakatwa mapanga baada ya kuvamiwa nyumbani, katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, usiku wa Jumatano iliyopita.

Taarifa ya Wizara hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Wizara hiyo, Erasto Ching’oro kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana ilisema wizara hiyo inalaani vikali mazingira ya mauaji ya watu hao wa familia moja, ambapo wauaji walivamia nyumba ya mama mjane na kumuua yeye mwenyewe, na watu wengine sita wakiwemo watoto watatu.
“Wizara inapongeza utayari wa uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Jeshi la Polisi ambao waliweza kufika sehemu ya tukio ili kufuatilia mauaji hayo. Ni imani ya Wizara kuwa Polisi kwa ushirikiano wa wananchi wa wilaya ya Sengerema wataweza kuwasaka watuhumiwa wa mauaji na kuwachukulia hatua kali.
“Wizara inawasisitiza wananchi kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwakamata watuhumiwa ili kuondoa hofu miongoni mwa familia za kijiji cha Sima na wilaya ya Sengerema. Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutarejesha imani na utulivu miongoni mwa wakazi wa Sengerema na hivyo kuweza kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa,” ilieleza.
Ching’oro alieleza katika taarifa hiyo kuwa Wizara inasisitiza kwamba kila binadamu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa Sheria za nchi. “Vitendo vya mauaji ya kikatili vinapotokea katika familia zetu vinasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanafamilia.
Mauaji hayo yanawakosesha amani wanafamilia na yanadhoofisha ari ya ndugu wa familia kufanya shughuli zao kwa amani,” aliongeza. Alisema Wizara inaomba wanafamilia waliopoteza ndugu zao kuwa na moyo wa subira katika kipindi cha majonzi makubwa, wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuwasaka watuhumiwa wa mauaji hayo.
Juzi taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Mkoa wa Mwanza, Atley Kuni aliyefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Kamanda wa Polisi Mkoa, Ahmed Msangi katika eneo la tukio, alisema watuhumiwa katika tukio hilo hawajajulikana.
Aliwataja waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Augenia Philipo (62), Maria Philipo (56), Yohana Mabula (20), Regina Aloyce (12), na Mkiwa Philipo (13) huku wengine wawili wakitambulika kwa jina moja moja la Donald na Samson.
Aidha, chanzo cha mauaji hayo ya kikatili hakijajulikana, ingawa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Zainab Telack alisema huenda mauaji hayo inawezekana yakawa ni ya kulipiza kisasi.