Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.
AHADI ya Rais John Magufuli ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji kwa ajili ya kusaidia vikundi vya wajasiriamali wanawake na vijana, imeanza kutekelezwa baada ya Wizara ya Fedha na Mipango kutenga Sh bilioni 59.6 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2016/17.

Wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Dk Magufuli aliahidi kuwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), atatoa kwa kila kijiji Sh milioni 50 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.
Katika Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyowasilishwa jana bungeni na Waziri Dk Phillip Mpango, inaomba kuidhinishiwa Sh trilioni 9.5 ambazo miongoni mwa hizo, zimo Sh bilioni 59.5 za kutekeleza ahadi ya Dk Magufuli.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika taarifa yake iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege (CCM) ndiyo iliyoibua hoja hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, iliyonukuu kitabu cha mafungu ya fedha, serikali imetenga Sh bilioni 59.5 kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa nchi nzima.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, ilipofanya tathmini ya vijiji na mitaa ya Tanzania Bara tu, ikakuta kuna vijiji na mitaa 19,600, ambayo ili kila kimoja kipate hizo fedha, kunahitajika Sh bilioni 980. Kwa uchambuzi uliofanyika, fedha zilizotengwa katika bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo kwa mwaka ujao wa fedha ni asilimia sita tu ya mahitaji, ambayo inatosha kutekeleza ahadi hiyo kwa ajili ya vijiji 1,190 tu, kati ya vijiji 19,600 vya Tanzania Bara.
Hali hiyo imelalamikiwa na wabunge wachache waliopata nafasi za awali kuchangia hoja hiyo, ambao walisema kwa utengaji huo wa fedha za utekelezaji wa ahadi hiyo waliodai iliwasaidia kupata kura, hawajui watarudije majimboni kuonana uso kwa uso na wapiga kura wao.
Akizungumzia masuala mengine, Dk Mpango alisema kati ya fedha ambazo wanaziomba ziidhinishwe na Bunge, Sh trilioni nane zikipangwa kutumika kuhudumia deni la Taifa. Alisema Idara ya Deni la Taifa yenyewe imeombewa Sh trilioni 8.009 na kati ya hizo, Sh bilioni tisa ni za kulipia mishahara na Sh trilioni nane za kuhudumia Deni la Taifa.
Dk Mpango alisema wizara hiyo imejipanga kuchukua hatua madhubuti za kujenga Taifa linalojitegemea kwa kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Katika kutimiza azma hiyo, Dk Mpango alisema moja ya hatua zinazochukuliwa na serikali ni kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016/2017 mpaka 2020/2021.
Kuhusu jukumu moja muhimu la wizara hiyo la ukusanyaji mapato, alisema wizara hiyo itajielekeza katika kusimamia matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato.
Pia inatarajia kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi na kuiingiza katika mfumo wa kodi na hivyo kupanua wigo wa kodi, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za serikali ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Serikali pia imejipanga kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na kuboresha usimamizi wake chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutokana na uzoefu wa mamlaka hiyo na mifumo yake ya ukusanyaji mapato nchi nzima.
Alisema pia serikali imejipanga kuendelea kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija, kuimarisha usimamizi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara bandarini na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa.
Mashirika ya umma Kuhusu mashirika ya umma, alisema wizara pia ilifanya uperembaji (monitoring and evaluation) kwenye taasisi na mashirika ya umma 55 yaliyobinafsishwa kwa lengo la kukagua ufanisi na kuhakiki utekelezaji wa masharti kulingana na mikataba ya ununuzi kwa mujibu wa agizo la Rais Magufuli wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11.
Aliyataja baadhi ya mashirika hayo ni Mwanza Textile, Shinyanga Meat, Ilemela Fisheries, Manawa Ginneries, Blanket Manufacturing, Mtwara Cashewnut Factory, Likombe Cashewnut, Newala I Cashewnut Factory, Newala II Cashewnut Factory, Mtama Cashewnut Factory, Mufindi Pyrethrum Factory, TTA Dabaga, Mufindi Tea Company, Ludodolelo Pyrethrum Factory na Mahenye Farm.
“Kilichobainika ni kuwa baadhi ya wawekezaji kushindwa kutekeleza masharti ya mikataba hususan kuwekeza kwa kuzingatia mpango wa uwekezaji uliokubalika kati ya serikali na wawekezaji,” alisema Dk Mpango.
Alisema baada ya uperembaji huo, wizara imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuwaita wawekezaji wote waliobainika kutotekeleza mikataba ya mauzo; kutoa notisi ya kusudio la kuvunja mikataba ya mauzo kwa baadhi ya wawekezaji na kuvunja mkataba wa mauzo na wawekezaji.
“Kusaidia kutatua baadhi ya changamoto ambazo zimesababisha kutotekelezwa ipasavyo kwa mikataba ya mauzo ikiwemo kutokuwepo mipango wa uwekezaji na kuwapongeza baadhi ya wawekezaji ambao wameendelea kufanya vizuri katika kuendeleza mali walizonunua na kuchochea shughuli za kiuchumi na hatimaye kuchangia kwenye Pato la Taifa,” alieleza waziri huyo.
Katika makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, serikali imejipanga kusimamia matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato. Hivyo ameagiza mifumo na vifaa vya kielektroniki kuanzia mwaka ujao wa fedha, vitumike katika utoaji wa stakabadhi za tozo, faini, ada na malipo mengine yote ya Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Wakala wote wa Serikali.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, vifaa hivyo vitatumika katika malipo ya faini za mahakamani, faini za usalama barabarani, viingilio kwenye mbuga za wanyama na vibali vya kuvuna maliasili.
Aidha, serikali imeamua kufanya uthamini wa majengo kwa mkupuo, ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi za majengo na usimamizi wake kuwa chini ya TRA kuanzia mwaka ujao wa fedha 2016/2017.