Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.
RAIS John Magufuli ametuma ujumbe bungeni kuwa yeye ni mbunge namba moja na anataka mapato yake yote yakatwe kodi stahiki, hatua inayofuata ni kutoachwa kwa mtu yeyote katika suala la kodi ya mapato.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitangaza ujumbe huo wa Dk Magufuli kwamba alipewa mapema alipopeleka pendekezo la kukata kodi ya mapato katika kiinua mgongo cha wabunge. Kwa mujibu wa Dk Mpango, kabla hata ya kuwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alipeleka mapendekezo hayo ya kwa Rais Magufuli.

“Nataka niwaambie, nilipopeleka hili (kukata kodi kiinua mgongo cha wabunge) kwa Rais, alinishangaa na kisha akasema yeye ni Mtanzania na ni lazima Watanzania wote walipe kodi kwa ajili ya kuendeleza nchi yao. “Rais alisema yeye ni mbunge wa kwanza wa Tanzania mpya na anapenda awe wa kwanza kukatwa kodi stahiki katika mapato yake, hivyo sasa kiinua mgongo cha Rais kitakatwa kodi,” Dk Mpango aliwaambia wabunge wenzake jana wakati akifanya majumuisho ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17.
Kutokana na kauli hiyo ya Rais, Dk Mpango alisema hata Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa viinua mgongo vyao lazima vikatwe kodi. Alimgeukia Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, akamwambia kuwa na yeye lazima akatwe kodi kisha akawageukia mawaziri, akawakumbusha kuwa wao ni wabunge na kwa dhamana waliyopewa kuwa mawaziri, wanapaswa kuongoza kwa mfano katika kukatwa kodi ya mapato katika mapato yao.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Dk Mpango, inashuka katika ngazo zote za uongozi, kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, ambao nao pia kiinua mgongo chao, lazima kikatwe kodi. Akifafanua hatua hiyo ya serikali kukata kodi ya mapato kwa kila mtu, waziri alisema sheria inataka vyanzo vyote vya mapato vikatwe kodi na kiinua mgongo ni moja ya vyanzo vya mapato vinavyotambulika na sheria hiyo.
Alisema kila Mtanzania amekuwa akikatwa kodi hiyo isipokuwa wachache na hatua hiyo ya serikali inalenga kutoa haki sawa katika utozaji kodi kwa jamii yote. Baada ya muda, Naibu Spika, Dk Tulia alitania mbona Mwanasheria Mkuu George Masaju na Spika Job Ndugai hawajatajwa au wao wamesamehewa; na katika jibu la ishara, Dk Mpango alionesha kutikisa kichwa kueleza kuwa hawajasamehewa, bali nao watakatwa kodi hiyo.
Kuhusu sababu ya kuwasilisha mapendekezo hayo ya kodi wakati kiinua mgongo cha wabunge kitakatwa kodi wakati wakimaliza kipindi chao cha miaka mitano, Dk Mpango alitoa sababu mbili za hatua hiyo. Mosi, alisema anakusudia kujenga utaratibu wa kutabirika kwa mapato ya serikali, lakini pili akitokea mbunge akakoma ubunge kabla ya wakati huo, makadirio yake ya kiinua mgongo, yakatwe kodi hiyo.
Ugumu wa kazi yake Dk Mpango alisema hoja hiyo ya kiinua mgongo, ilizungumzwa kwa hisia kubwa na wabunge, wengine walimwambia kuwa aliwabipu na wao wakaamua kumpigia, wengine wakasema ameshika pabaya panapouma na wengine wakamwambia hajui uchungu wa jimbo, kwa kuwa yeye ni Mbunge wa Kuteuliwa. Waziri huyo wa Fedha na Mipango alisema changamoto moja ya wizara anayoiongoza ni kulazimika kuwa mkweli kwa kueleza kinachowezekana na kisichowezekana ili kujenga nchi.
Kuvuja jasho Alisema Bajeti ya Serikali aliyoiwasilisha, inalenga kuanzisha safari aliyoiita kuwa safari ngumu ya kuitoa Tanzania katika kutegemea kilimo duni kwenda kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati. Dk Mpango alisisitiza kuwa ndio maana baada ya Bunge kuipitisha bajeti hilo, utekelezaji wake utakuwa wa kuvuja jasho huku akisema kwa hali ya nchi iliyopo Watanzania wana mambo mawili tu ya kuchagua.
Jambo la kwanza, alisema ni kuendelea utendaji wa mazoea ambao kwa mtazamo wake suala hilo halikubaliki na haliwezi kuwa uchaguzi wa Watanzania; na jambo la pili ni kufanya kazi na viongozi wawe wa kwanza kuonesha mfano katika kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu. Kutokana na uchaguzi huo wa pili, alisisitiza kwa wizara zote, mashirika ya umma na taasisi zinazojitegemea kuhakikisha wanakusanya mapato ya serikali, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuzuia ongezeko la madeni.
Alisema Watanzania lazima wafikie malengo ya kukusanya mapato ya serikali na kupeleka katika maendeleo ya wananchi kwa kuwa Tanzania ya sasa inazo akili za kutosha na rasilimali za kutosha kutoa taifa hapa lilipo kwenda uchumi wa kati. Bajeti ya CAG Kuhusu hoja ya bajeti ndogo katika Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk Mpango alisema ukomo wa fedha za matumizi ya kawaida katika serikali nzima, uliwekwa na serikali ili kupata fedha za kupeleka katika maendeleo.
Alisema kabla ya kuweka ukomo huo, kulifanyika uchambuzi wa fedha za matumizi mengineyo ndani ya serikali nzima na kubaini uwezekano wa kuwa na matumizi madogo ambayo hayataathiri utendaji wa serikali. Dk Mpango alisema hata ofisi ya CAG ilifanyiwa uchambuzi na bajeti waliyotengewa ilithibitika kuwa hatashindwa kufanya kazi na atakuwa na uwezo wa kukabiliana na dharura bila kuathiri uhuru wake.
Aliwahakikishia wabunge kuwa yeye atakuwa wa mwisho kumzuia CAG kufanya kazi yake ya kukabiliana na mchwa wa fedha za umma na kusisitiza kuwa hata uhuru wa CAG unalindwa na katiba na yeye hawezi kuuingilia. Jana jioni wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walipitisha Bajeti hiyo ya Serikali kwa mwaka 2016/17 baada ya wale wa vyama vya upinzani kususia Bunge wakimpinga Naibu Spika Dk Tulia.
Kwa mujibu wa Katiba, Bunge linatakiwa kuwa na wabunge 393, lakini waliopo sasa ni 389. Walioingia ukumbini walikuwa 252 na ambao hawakuwapo ni 137. Kura za Ndiyo zilikuwa 251, hakuna kura ya Hapana wala Kutoamua katika upitishaji huo wa bajeti ambao kwa mujibu wa sheria inapita endapo itaungwa mkono na nusu ya wabunge waliopiga kura.