Rais John Magufuli akizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress aliyemtembelea Ikulu, Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).
SERIKALI ya Marekani imetangaza kuwa itatoa dola za Marekani milioni 800 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Uthibitisho wa kutolewa kwa msaada huo, umetangazwa na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli katika Ikulu ya Dar es Salaam jana.

Balozi Childress alisema kutolewa kwa fedha hizo ni uthibitisho kuwa kutotolewa kwa fedha za awamu ya pili ya Mradi wa Changamoto za Milenia (MCC-2), hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Marekani, ikiwemo utoaji wa misaada ya maendeleo.
“Tumezungumza mambo kadhaa, na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia shirika letu la misaada la USAID tunatarajia kutiliana saini mkataba wa zaidi ya dola milioni 400 kwa ajili ya mwaka ujao, pia tumezungumza kuwa kutakuwa na dola milioni 800 zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali na hii haihusiani na MCC,” alisema Balozi Childress muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.
“Ukweli ni kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi kuhakikisha haya yanafanikiwa,” alisema. Naye Rais Magufuli alisema Serikali yake ya Awamu ya Tano, itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Marekani na kwamba fedha za msaada kutoka Marekani ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.
“Amekuja kutuhakikishia kwamba watatoa hela kwa ajili ya Tanzania na anasema sasa hivi watatoa zaidi ya dola milioni 800, na mkataba mwingine tunaweza tukasaini hata kesho wa dola milioni 410.
“Anasema kutotoa hela za MCC hakuna maana kupotea kwa urafiki wa Tanzania na Marekani, urafiki wa Tanzania na Marekani upo pale pale na sasa wanaongeza hela nyingi zaidi katika kuonesha kwamba juhudi za Hapa Kazi Tu zinaendelea,” alisema Rais Magufuli.
Miezi michache iliyopita, Marekani ilitangaza kusitisha utoaji wa fedha za miradi ya MCC- 2 ikitoa sababu mbili, ikiwamo kupitishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mitandao na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli jana alikutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Didier Reynders na kuzungumzia kuendeleza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo hususan katika maendeleo.
Pamoja na kuzungumzia miradi ya ushirikiano inayotekelezwa kati Tanzania na Ubelgiji katika mkoa wa Kigoma, viongozi hao pia walikubaliana kuongeza ushirikiano katika biashara na uwekezaji, huku Didier Reynders akiahidi kushawishi kampuni nyingi za Ubelgiji kuja kuwekeza nchini.
Aidha, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Italia nchini, Luigi Scotto aliyemaliza muda wake wa miaka mitatu. Wakati huo huo, Rais Magufuli jana alitia saini kitabu cha maombolezo katika Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Nchi za Kiarabu ya Saharawi, Mikocheni jijini Dar es Salaam kutokana na kifo cha Rais wa nchi hiyo, Mohamed Abdelaziz aliyefariki dunia Jumanne iliyopita.
Rais Magufuli ambaye alipokelewa na Balozi wa Saharawi nchini, Brahim Salem Buseif alisema Abdelaziz ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Polisalio Front, atakumbukwa kwa juhudi zake za kupigania ukombozi na Uhuru wa Saharawi.