Mahakama kuu ya Arusha
MLALAMIKIWA wa kwanza katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Longido mkoa wa Arusha, Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema), ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa anajua kusoma na kuandika Kiswahili, lakini hajui kusoma na kuandika Kiingereza.

Shahidi huyo wa kwanza kwa upande wa wajibu maombi, alisema hayo jana mbele ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Bukoba, Silvangirwa Mwangesi aliyesikiliza kesi hiyo wakati akihojiwa na Wakili Dk Masumbuko Lamwai.
Wakili Lamwai alitoa mahakamani hapo fomu iliyojazwa na Nangole, ambayo ameiprint kutoka katika tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ikiwa na picha na kuiwasilisha mahakamani hapo, na aliomba kuisoma mbele ya Jaji Mwangesi na inaonesha alisoma wapi mbunge huyo elimu ya sekondari.
Nangole aliisoma na kuonesha kuwa alisoma katika Shule ya Arusha Sekondari mwaka 2008 hadi 2011, wakati katika mahakama hiyo amesema hakusoma sekondari na wala hajui kusoma na kuandika Kiingereza.
Wakili Lamwai alimuuliza Nangole kama katika mikutano ya kampeni yeye na wafuasi wake, walitumia lugha za kashfa dhidi ya mgombea wa CCM, Dk Stephen Kiruswa, ambapo alikana kutoa lugha hizo.
Lakini, alipopewa hati ya kiapo chake na kutakiwa kusoma, ilionesha kutamka maneno hayo katika mikutano ya hadhara na katika kiapo chake. Nangole alipotakiwa kusema mahakama iamini nini ili itoe maamuzi kwa kiapo alichoandika au alichosema mahakamani hapo, Nangole alikaa kimya na Jaji Mwangesi alimwamuru kujibu swali, ndipo aliposema hajui.
Aidha, Dk Lamwai alimuuliza katika timu yake iliyokuwa na watu 14, kama alihudhuria mikutano yote ya kampeni 68, Nangole alisema siyo yote alihudhuria na mingine ilikuwa ikihutubiwa na Karisti Lazaro wakati huo akiwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha, sasa ni Meya wa Jiji la Arusha na Isack Joseph maarufu kwa jina la Kadogoo, sasa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.
Shahidi huyo alioneshwa picha na wakili Lamwai, ambayo ni ushahidi uliotolewa kama kielelezo P5c cha matukio ndani ya chumba cha kuhesabu kura, akiwemo mbunge na wafuasi wake wakiwa mbele ya kompyuta iliyovurugwa ;na kumuuliza ni kwa nini walikuwa wengi ndani ya chumba hicho kinyume cha sheria, shahidi alijibu hajui.
Aliulizwa na Wakili Lamwai, kama kulikuwa na wafuasi wengi wa CCM ndani ya chumba hicho, mbunge huyo alikiri kutokuwepo katika chumba hicho wafuasi wa chama hicho tawala.
Baadhi ya mahojiano kati ya Wakili Lamwai na shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mjibu maombi yalikuwa: Wakili: Kwa nini hukusoma kiapo chako? Shahidi: Naumwa macho.
Wakili: Sio kuwa hujui kusoma Kiingereza?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Sekondari ulisoma wapi?
Shahidi: Sikusoma.
Wakili: Elimu ya sekondari ulisoma shule gani?
Shahidi: Sikusoma sekondari.
Wakili: Katika fomu yako uliyoandika siku unajiandikisha bungeni ambayo nimeiprint katika tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, hii hapa, inaonesha umeandika umesoma wapi sekondari? Katika shule ya Arusha sekondari.
Shahidi: Sijui mimi, sikuandika mimi hiyo.
Wakili: Unajua kusoma na kuandika Kiingereza?
Shahidi: Sijui.
Wakili: Kwa nini umesomewa kiapo chako kilichoandikwa Kiingereza na wakili wako, ni kwa sababu hujui Kiingereza?
Shahidi: Najua kusoma na kuandika Kiswahili.
Wakili: Unajua Kiingereza?
Shahidi: Kimya.
Jaji: Jibu swali. Mbona maswali ni rahisi tu pamoja na kwamba yanauma…jibu tu.
Shahidi: Sijui kusoma Kiingereza wala kuandika.
Wakili: Katika maisha yako yote ya miaka 23 uliyokuwa CCM ulikuwa na vyeo mbalimbali.
Shahidi: Ndio. Wakili: Ulihama CCM kumfuata Edward Lowassa Chadema sio?
Shahidi: Ndio, unauliza jibu.
Wakili: Ulifanya hivyo ili ubebwe na Lowassa katika ubunge Longido sio?
Shahidi: Ndio jibu unalo.