Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili, imeboresha huduma zake ambapo kuanzia Julai Mosi mwaka huu itakuwa inatoa chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa hospitalini hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma hospitalini hapo, Aminiel Aligaesha alisema hospitali imeingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa wote wanaolazwa.

Alisema huduma hii imelenga kuwaondolea ndugu wa wagonjwa usumbufu na gharama za usafiri wakati wanapokwenda kuwaona waliolazwa karibu mara tatu kwa siku katika hospitali hiyo.
Badala yake, chakula kitaandaliwa hospitalini hapo. Ili kutoa huduma hiyo, kutakuwa na kuchangia gharama kidogo ambapo, mgonjwa atalazimika kutoa Sh 10,000 kwa kulazwa, Sh 10,000 kumwona daktari na Sh 30,000 kwa chakula.
Gharama hizo ni kwa siku 5 ambazo ni jumla ya Sh 50,000. Aligaesha alisema hospitali hiyo inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu. “Hospitali inataka kuwaondolea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama kubwa hususani usafiri wa kuja hospitalini mara tatu kwa siku,” alisema.