Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
SEMINA kuhusu Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma, iliyofanyika bungeni jana, iligeuka sehemu ya kupashana ukweli kuhusu hali ya kukosekana kwa uadilifu kati ya viongozi wa jamii na wa dini, wataalamu wa ununuzi na jamii nzima.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya wabunge kumaliza kusikiliza mada, iliyotolewa na Kamishna wa Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Fredrick Mwakibinga ambaye kabla ya kumaliza mada yake, aliwaachia wabunge hao changamoto kuhusu maadili katika jamii.
Dk Mwakibinga katika changamoto hiyo, alisema watumishi wakiwemo wataalamu wanaotumia vibaya nafasi zao katika suala la manunuzi ya umma, ndio wanaosifiwa sana katika jamii. Alitoa mfano wa wazazi kwamba wamekuwa wakiwathamini watoto wanaotumia nafasi zao vibaya katika ununuzi wa umma, kwa kuwa wanapeleka kitu nyumbani kwa kuwaona wao ni watoto wazuri kuliko ambao hawafanyi hivyo.
Kamishna huyo alisema hata makanisani, watu waliotumia vibaya nafasi zao na kufanya madudu katika ununuzi wa umma, ndio wamekuwa wakipewa viti vya mbele na kushauri ili hali ibadilike, pamoja na kurekebisha sheria ili kuongeza udhibiti, ni lazima jamii ibadilike na kukemea ukosefu wa maadili katika jamii.
Wabunge, madiwani majambazi Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy (CCM) alihoji kamishna huyo ameajiriwa lini serikalini kwa maelezo kuwa mada aliyotoa, imejitosheleza kwa kuwa ameeleza namna anavyojua wizi karibu wote serikalini.
Alitoa mfano suala la ununuzi wa magari, ambalo Dk Mwakibinga alizungumzia katika kipengele kinachotaka serikali kununua magari kwa jumla kutoka kwa mtengenezaji badala ya kupitia kwa wakala ili kupata bei nafuu, suala ambalo Kessy alisema amelipigia kelele siku nyingi, lakini halikuwa likifanyiwa kazi.
Kessy alisema gari moja la serikali, limekuwa likinunuliwa kwa bei kubwa, ambayo inaweza kununua magari ya aina hiyo matatu kwa kutumia fedha hiyo hiyo. Akizungumzia maombi ya wabunge kuingia katika kamati za zabuni katika halmashauri ili wadhibiti ununuzi mbovu unaofanywa na kamati hizo kwa kutoa zabuni kwa walioitwa watoto wa wajomba, Kessy aliunga mkono maombi hayo, lakini akahadharisha kuwa hata wabunge na madiwani si malaika.
Alisema wako wabunge na madiwani majambazi ambao wanaweza kuingia katika kamati hizo wakiwa na wazabuni wao na kusisitiza umuhimu wa kudhibiti tabia hiyo, ikiwezekana akibainika mbunge kaingia katika kamati hizo akiwa na wazabuni, awajibishwe.
Kujifanya wajuaji
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) aliunga mkono suala la marekebisho ya sheria hiyo, akisema kila mbunge anaunga mkono kuwa sheria iliyopo ni mbovu, lakini akahoji ilikuwaje wabunge walipitisha sheria mbovu kama hiyo ambayo sasa wamerudishiwa wairekebishe.
Msigwa alisema tatizo la wabunge, wanajifanya wanajua kila kitu na kutoa mfano kuwa akitokea mtaalamu wa nyuklia, akatoa mada bungeni kuhusu suala la nyuklia, utaona wabunge wakitaka kuchangia wakati hawajui chochote katika masuala hayo.
Uadilifu wenye shaka
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alisema ingawa hakuna sheria inayodumu daima, lakini kuna haja ya kuangalia namna ya kushughulikia tatizo la viwango vya uadilifu visivyoridhisha.
Makani alihadharisha kuwa kama suala la uadilifu na weledi halitapewa mkazo, sheria hiyo hata baada ya kufanyiwa marekebisho, haitaweza kufanya kazi. Alisema uadilifu mtu anaweza kuzaliwa nao, lakini weledi ni suala la mafunzo, hivyo akapendekeza marekebisho ya sheria hiyo, yaendane sambamba na marekebisho ya sheria ya maadili kwa kuwa wataalamu wamekuwa wakijinufaisha kwa kuangalia upenyo unaotolewa na sheria.
Dk Mwakibinga alizungumzia matokeo wanayotarajia kuyapata baada ya marekebisho ya sheria hiyo, kuwa ni pamoja na kupungua kwa tofauti ya bei zinazotumika katika ununuzi wa umma na bei ya soko.
Matarajio mengine ni kupungua kwa gharama na muda wa michakato ya ununuzi; kunufaika na matumizi ya viwango vya mahitaji ya serikali vilivyopitishwa; kujenga uwezo wa viwanda vya ndani, makundi maalumu ya jamii, kwa kuyaruhusu kuomba zabuni za umma na kuongeza ajira.
Pia marekebisho hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa taasisi za umma zinazojiendesha kibiashara, ambazo zitawekewa utaratibu maalumu na kuongeza mchango wa sekta ya ununuzi katika ukuaji wa uchumi.