kamanda_mwanza


MWANZA: Muuza duka la dawa baridi ‘famasi’ katika Kijiji cha Matara wilayani Kwimba, Stephen Ng’wanyi anasakwa na jeshi la polisi akituhumiwa kusababisha kifo cha Anna Martine (18) baada ya kudaiwa kumdunga sindano kwa lengo la kumtoa mimba.
Anna alidaiwa kufariki dunia Julai 20, mwaka huu majira ya 2:00 asubuhi, baada ya kudungwa sindano na muuza duka huyo ili kutoa ujauzito wa miezi mitatu aliokuwa nao.
Ilielezwa kuwa Julai 19, marehemu alikuwa akilalamika kuumwa tumbo kutwa nzima lakini kutokana na maumivu kuzidi aliamua kumweleza dada yake Anna Fabian kuwa alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu na alidungwa sindano ya kuutoa huku akimtaja Stephen Ng’wanyi.
Hali yake ilizidi kuwa mbaya na kusababisha dada yake marehemu kwenda kumwita Ng’wanyi ili aje kumpa matibabu mdogo wake nyumbani hapo, lakini baada ya kufika aliwashauri ndugu wa marehemu aondoke naye hadi  nyumbani kwake kwa matibabu zaidi.
Kutokana na maombi hayo ndugu waliridhia Ng’wanyi kuondoka na Anna hadi kwake na muda mfupi baadaye alirejea na kuwaeleza ndugu hao kuwa mgonjwa alifariki dunia na baada ya kuwaambia alitoroka.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Augustino Senga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa jeshi hilo linamsaka muuza duka huyo kwa udi na uvumba ili afikishwe mahakamani kwa kosa la mauaji.
“Jeshi la polisi lipo kwenye msako kuhakikisha linamkamata mtuhumiwa huyo anayedaiwa kusababisha kifo cha Anna na kumfikisha mahakamani ingawa upelelezi unaendelea na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa uchunguzi,” alisema Senga.
Kaimu kamanda huyo wa polisi alitoa onyo kwa wananchi wa Jiji la Mwanza hasa wasichana, kuwa kutoa mimba bila sababu za kitabibu ni kosa la jinai na kinyume cha sheria na kuwashauri kutofanya hivyo.
Pia aliwataka wamiliki na wauzaji wa maduka ya dawa baridi wafanye biashara hiyo kwa kuzingatia taaluma yao na kwa mujibu wa masharti ya leseni zao yanavyoelekeza na si vinginevyo.
Na Mashaka Baltazar, RISASI Mchanganyiko