Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amewataka Watanzania wasichezee amani kwa kuwa Tanzania ni nchi pekee iliyobakia kuwa kisiwa cha amani.
“Tusichezee amani. Tuidumishe amani yetu kwani kuna watu walijitoa mhanga kupigania amani hiyo na kuifikisha nchi hapa ilipo,” alisema Rais Magufuli mjini hapa jana alipohutubia maelfu ya wakazi wa Dodoma na Watanzania katika sherehe ya Siku ya Mashujaa.

Rais Magufuli aliyeshangiliwa na wananchi waliokuwa wakipunga bendera ndogo za Taifa baada ya kupanda jukwaani, alisema kuwa wakati tunaadhimisha Siku ya Mashujaa tukumbuke wapo watu walikubali roho zao zipotee.
Alitoa mfano wa waliopigania ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika kama Msumbiji, Namibia, Angola, Comoro na Afrika Kusini. Wengine ni waliopigana vita ya nduli Iddi Amin wa Uganda mwaka 1977, wakati nduli alipovamia Tanzania na wakati wa Mapinduzi kisiwani Zanzibar mwaka 1964.
Aliwataja mashujaa wengine wa Taifa ambao hawawezi kusahaulika kwa mchango wao mkubwa katika ukombozi wa nchi kuwa ni Baba wa Taifa , Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amaan Karume wa Zanzibar.
Alisema waasisi hao walijitahidi kuifikisha nchi hapa ilipo.
“Tanzania imekuwa na amani na utulivu kwa sababu wapo watu waliojitoa mhanga kuipigania. Tudumishe amani yetu. Hawa wenzetu waliotangulia, hawakujali dini zao na makabila yao. Walijitahidi kuwaunganisha Watanzania wote,” alisema Rais Magufuli na kuwataka Watanzania wasichezee amani na asitokee wa kuichafua kwani kila mmoja ana wajibu wa kuidumisha. Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliwataka Watanzania kulinda umoja na amani ya nchi.
Aliwataka kuendelea kumuombea dua Rais Magufuli ili awe mwepesi katika kutekeleza yote anayodhamiria kwakuwa amepewa dhamana kubwa ya kuongoza Watanzania zaidi ya milioni 40.
“Tuache ushetani, tuache ubilisi, tushughulike na yale yanayotuhusu sisi wenyewe, watoto wetu na vizazi vyetu. Tudumishe utulivu na kupendana. Heri na amani haiji bila kupatikana usawa,” alisema na kuongeza kuwa Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa watu, anayepigania watu wanaokosa haki, wanaoonewa na wanaofanyiwa fitna.
Alisema amani ni kitu muhimu sana hivyo Watanzania wafunge masikio wasisikie mabalaa na machafuko yanayotokea katika nchi jirani. Aliongeza kuwa, Mungu katujalia amani hivyo tuidumishe ili asitokee mtu kuiharibu.
“Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Huko nje maguu yanavunjika na yataendelea kuvunjika,” alionya Mwinyi. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema atashirikiana na Rais Magufuli kuimarisha amani ya Tanzania.
Alisema anafahamu uwezo, nia, ari, jitihada na kasi ya Rais Magufuli ya kuipeleka Tanzania kuwa nchi yenye matumaini na maendeleo makubwa.
Akitoa dua katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Kaimu Shehe wa mkoa wa Dodoma, Ahmed Said, alisema Watanzania wanathamini mchango mkubwa walioutoa mashujaa waliopigania nchi na kwamba mchango wao utaendelea kuthaminiwa.
Alisema umoja na amani havikushuka nchini kama mvua, bali wazee na askari walitoa jasho na kupoteza maisha kwa ajili ya nchi ndio waliosababisha viwepo.
Alisema Watanzania hawawezi kusahau waasisi walioongoza mapambano wakiwemo Mwalimu Julius Nyerere, Shehe Abeid Amaan Karume na Rashidi Kawawa.
“Tunamuomba Mungu aendelee kuilinda nchi yetu na kudumisha amani, utulivu na umoja uliopo,” alisema Shehe Said. Pia, Shehe Said aliwataka Watanzania waendelee kumuombea Rais Magufuli awe na moyo wa ujasiri, subira na afya njema ili aweze kuongoza nchi kama ilivyokusudiwa.
Aliomba Mungu awaepushie shari viongozi wanaomsaidia Rais Magufuli kuongoza Serikali. Shehe huyo aliomba Mungu ailinde Tanzania na Watanzania kwa ujumla na pia aubariki Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili uendelee kudumu.
Mchungaji Leonard Mtaita akifanya maombi kwa niaba ya Umoja wa Makanisa ya Kikristo (CCT), alisema waasisi wa Taifa wametoa mchango mkubwa katika kujenga na kudumisha amani.
Aliwataka Watanzania kudumisha upendo na amani kama njia ya kuwaenzi. Mtaita aliwahimiza Watanzania waendelee kumuombea Magufuli aendelee kuwa na afya njema, hekima na busara ili kuwatumikia Watanzania. Alimsifu Rais kwa kuwatumikia kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
Padri Onesmo Wisi alifanya maombi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema Watanzania wanafurahia amani ambayo waasisi na askari wetu waliipigania. Aliwahimiza kuwa na umoja ili kulinda amani iliyopo na kujiepusha na uchochezi wa kisiasa, ambao mwisho wake ni vurugu.
Katika maadhimisho hayo, shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuweka silaha za asili za mashujaa na maua kwenye mnara, ambapo Rais Magufuli aliweka mkuki na ngao na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange aliweka sime. Kiongozi wa Mabalozi nchini, Balozi Ambrosio Lukoki aliweka shada la maua.
Lukoki ni Balozi wa Angola nchini. Meya wa Dodoma, Jaffar Mwanyemba aliweka upinde na mshale na Mwenyekiti wa Tanzania Legion, Rashid Bakar Ngonji aliweka shoka.
Pia mizinga miwili ilipigwa katika sherehe hizo zilizopambwa na gwaride maalumu. Maelfu ya wakazi wa Dodoma walihudhuria sherehe hizo. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa sherehe za Siku ya Mashujaa kufanyika nje ya Dar es Salaam.