|
SERIKALI imeanza mkakati mpya wa kuandikisha wananchi waliopo kwenye vijiji na vitongoji kwa njia ya kielektroniki ili kupata takwimu sahihi zitakazosaidia utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Pia mfumo huo utatambua watu wadanganyifu ambao wamekuwa wakidanganya wanakotoka, ikiwemo wezi na majambazi ambao ni lazima waeleze wanakoishi, wanakotokea, jina la mkuu wa kaya wake na namba ya utambulisho wake.
Mfumo huo ambao utasaidia kujua watoto waliozaliwa na watu waliokufa, taarifa zitakazotolewa kwa Mtendaji wa Serikali za Mitaa ambaye atarekodi kwa njia ya simu na taarifa hizo zitafika moja kwa moja kwenye Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambao wataweka kumbukumbu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mussa Iyombe alisema kuwa ili kufanikisha uhakiki huo, serikali imetenga Sh bilioni 1.6 wakati wahisani wamechangia Sh bilioni 1.4.
Iyombe alisema takwimu hizo pia zitaisaidia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Udhamini na Ufilisi (RITA) katika utoaji wa vitambulisho na hati za kuzaliwa na vifo. Aidha, alisema lengo ni kuhakikisha kila mtu anatumia kitambulisho kimoja pekee kumtambulisha kuliko ilivyo sasa kwamba watu wanakuwa na vitambulisho zaidi ya saba.
"Hii itakuwa dawa ya kuwatambua majambazi, wezi, wahamiaji wa kigeni na hata watoto wanaozaliwa na vifo. Mtendaji wa mtaa atakuwa anarekodi taarifa hizo kutoka kwa mkuu wa kaya ambapo ataeleza watoto waliokuwepo, wapangaji wangapi. Mpangaji pia akitaka kuhama ni lazima aseme anakwenda wapi ili aweze kupokelewa anakokwenda," alisema Iyombe.
Kwa mujibu wa Iyombe, awali walikuwa wanatumia madaftari katika kusajili watu waliopo kwenye vijiji na vitongoji hali ambayo ilikuwa na changamoto kutokana na watendaji wengine kutojaza taarifa za wakazi wao.
Alisema kuwa serikali imekuwa ikikosa taarifa muhimu za awali na kuamua kuanza mfumo huo ambao utafanyika nchi nzima kwa miaka miwili.
Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Chuo cha Takwimu Kusini mwa Afrika waliamua kuanza mfumo huo Kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo na kwamba wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Alisisitiza kuwa sensa ya mwaka 2022 itatumia taarifa zitakazokusanywa kwa kipindi cha miaka miwili ijayo ili kuondoa ubabaishaji uliokuwa unafanywa awali.
Pia alisema kwa sasa nchi inapopatwa na janga lolote hutumia taarifa zisizo rasmi kwa ajili ya kutoa msaada, hivyo vijiji vingine kuona kuwa serikali haiwasaidii wanapopatwa na matatizo. Kwa upande wake, Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Amina Said alisema kuwa kabla ya sensa nyingine Tamisemi wawe wamemaliza uhakiki wa watu kutumia mfumo huo.
Alisema kuwa katika nchi zinazotumia mfumo huo, hakuna sensa kwa kuwa wanazo taarifa sahihi za watu wao. "Mfumo huu utaingiza watu wapya na kuwatoa waliokufa ili kufanya makadirio mazuri yatakayosaidia kuwatambua watu wote ikiwemo wavamizi pia itapunguza muda wa kupata idadi ya watu," alisema Said.
Pia alisema kuwa wasimamizi wakubwa wa mfumo huo ni Tamisemi hivyo wananchi washirikiane na viongozi wao kutoa taarifa sahihi ili kuwatambua na si kwa nia mbaya. Hata hivyo alisema kuwa kupitia mfumo huo itasaidia wanafunzi kuandikishwa kwenye shule zilizopo maeneo yao kuliko kuandikisha watoto nje ya kata ya mwanafunzi.
Aliwataka wanasiasa na viongozi wote watambue na kushiriki katika kuwaelimisha wananchi na kuwatoa hofu kuhusu mfumo huo ili kutoa huduma bora za jamii. Naye, Diwani wa Kata ya Mapinga Bagamoyo ambaye kata yake imefanyiwa majaribio, Ibrahim Mbonde alisema kuwa ameandikisha kaya 341 kwa njia ya kielektroniki na kwamba mfumo umeonesha mafanikio makubwa.
Mbonde alisema serikali imeondoa gharama za kununua madaftari kwa ajili ya uhakiki ambavyo vilikuwa havijazwi. Alisema walikuwa wanashindwa kupata taarifa za watu ikiwemo wajawazito wanaojifungulia nyumbani na wanaokufa na kusababisha kuwepo kwa takwimu za kukisia.
"Kila kaya inakuwa na namba yake hivyo mtu anayeenda kuhakiki na kutaja namba tofauti hutambulika kuwa mdanganyifu. Kwa mfano kwangu watu wapo 23,000 ni lazima tungenunua madaftari mengi, njia hii itasaidia kuleta maendeleo ya Taifa," alisema Mbonde.
0 Comments