Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
JESHI la Polisi mkoani hapa limeanza kufanya doria mchana kwa kutumia magari kwa lengo la kujiweka sawa kukabiliana na vurugu zozote zitakazotokea.
Katika mitaa ya Dodoma jana asubuhi zaidi ya askari 200 wakiwa na magari 27 wakiongozwan na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lazaro Mambosasa walifanya doria na mazoezi kwa vitendo mchana.

Jambo hilo lilionekana kuzusha taharuki kwa wananchi kutokana na askari hao kuwa na silaha lilianza majira ya asubuhi saa moja mpaka saa saba mchana askari hao walipita mitaa kadhaa ya mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lazaro Mambosasa alisema hiyo ni kazi ya kuuweka sawa Mkoa wa Dodoma kwa wale ambao wataleta vurugu katika siku za hivi karibuni.
Alisema doria kama hizo huwa zinafanyika usiku, lakini sasa wameamua kufanya mchana ili kuliweka jeshi vizuri. Tulikuwa tunajaribisha kama vyombo vyetu vipo vizuri na hili ni zoezi la kawaida tu.’’
Hatukuwa na doria ya kutembea kwa miguu tuliamua kutumia pikipiki na sehemu ya magari yetu kuuweka mji katika hali ya usalama,” alisema. Alisema sababu ya kufanya hivyo ni kuendelea kufanya wakazi wa Dodoma kuendelea kuwa na usalama huku akidai hapo ni makao makuu ya Chama na Serikali.