Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Julai, 2016
amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) Dkt. Frannie Leautier katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma,
ambapo ameishukuru benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya
Tanzania  hususani kutoa mikopo
iliyowezesha ujenzi mkubwa wa barabara.



Pamoja na kuishukuru
AfDB Rais Magufuli ameiomba benki hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania
katika utekelezaji wa mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mpango
mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme utakaofanikisha ujenzi wa viwanda,
ujenzi wa barabara zinazounganisha ndani na nje ya Tanzania na kuunga mkono
juhudi za kukabiliana na rushwa.


Kwa upande wake
Makamu wa Rais wa AfDB Dkt. Frannie Leautier amempongeza Rais Magufuli kwa
juhudi kubwa alizozianza katika kujenga uchumi wa Tanzania, kukabiliana na
rushwa na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali na ameahidi kuwa benki
hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa mikopo ya masharti nafuu
itakayofanikisha mipango na miradi mbalimbali ya Tanzania.


"Tanzania ni
nchi ambayo inapata fedha kuliko nchi zote za Afrika katika mpango wa AfDB
kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Afrika,
hizi ni fedha ambazo zinatolewa kwa mkopo nafuu zaidi kuliko mikopo
mingine" Amesema Dkt. Frannie Leautier.


Dkt. Frannier Leautier
amebainisha kuwa AfDB inatarajia kuwa Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele
vitano vya benki hiyo ambavyo ni kusaidia uzalishaji wa nishati, utangamano wa
bara la Afrika, maendeleo ya viwanda, usalama wa chakula na kuboresha hali ya
maisha.


Aidha, Makamu wa
Rais huyo wa AfDB amesema kuanzia mwakani benki hiyo imepitisha miradi mikubwa
mitatu kwa ajili ya Tanzania ambayo ujenzi wa nyumba ya makazi, utoaji wa
mikopo vijijini kwa ajili ya kuendeleza kilimo na maeneo ya uchumi kupitia
benki ya CRDB na kukiendeleza Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Nelson Mandela
kilichopo Arusha ambapo benki hiyo itatoa Dola za Marekani Milioni 4.


Mazungumzo hayo
yamehudhuriwa na Mwakilishi Mkazi wa AfDB Dkt. Tonia  Kandiero, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Ashatu Kijaji.


Gerson
Msigwa


Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU


Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Frannie Leutier aliyemtembele Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma leo Julai 26, 2016. Kushoto ni ni Mwakilishi wa Benki hio nchini, Bi. Tonia Kandiero


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimwangalia  Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Frannie Leutier akisaini kitabu (Leadership in a Globalized World: Complexity and Risk) alichotunga kabla ya kumkabidhi Rais alipomtembele Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma leo Julai 26, 2016

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akipokea kitabu cha "Leadership in a Globalized World: Complexity and Risk: kutoka kwa mtunzi  Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Frannie Leutier alipomtembele Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma leo Julai 26, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Frannie Leutier  na ujumbe wake aliyemtembele Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma leo Julai 26, 2016. Wa tatu kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, wa tatu kulia ni Mwakilishi wa Benki hio nchini, Bi. Tonia Kandiero, kulia ni Mchumi Mkuu kutoka Idara ya Fedha za Nje Bw. Johannes Jovin akifuatiwa na Mkrugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Wizara mambo ya Nje Balozi Celestine Mushy. Kushoto ni Mshauri wa Rais Masuala ya Uchumi Profesa Longinus Rutasitara akifuatiwa na Mshauri wa Rais masuala ya Diplomasia Balozi Zuhura Bundala.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiagana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Frannie Leutier aliyemtembele Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma leo Julai 26, 2016. Katikati ni Mwakilishi wa Benki hio nchini, Bi. Tonia Kandiero