RAIS John Magufuli ametuma salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza maisha katika ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la Veta Dakawa tarafa ya Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa 11:30 jioni ya Juni 30 mwaka huu, ambapo watu watano walikufa papo hapo, baada ya malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta, kugongana na kuwaka moto.
Ajali ya pili ilitokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya Julai mosi mwaka huu, baada ya basi la kampuni ya Otta High Class, kupamia lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu saba mpaka jana.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza jana kuwa katika salamu hizo kwa wananchi waliofikwa na msiba huo, kupitia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe, Rais Magufuli alisema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa hizo. Alisema Taifa limepoteza nguvu kazi muhimu, na ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliwaotegemea.
“Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Steven Kebwe, naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na uwaambie naunga nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. “Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, amina,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia aliwaombea majeruhi wote waliolazwa hospitalini na wale wanaoendelea kupata matibabu wakiwa nyumbani, kupona haraka ili waendelee na kazi zao za kila siku.