Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt John PombeMagufuli akiwahutubiamamiayawakaziwa mji wa Dodoma mapema leo asubuhi waliojitokeza kushuhudia maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika kwenye uwanja waMashujaa, mjini Dodoma.PICHA NA MICHUZI JR-DODOMA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi watanzania kuwaenzi Mashujaa
kwa kudumisha Amani, Umoja na Utulivu uliojengwa na mashujaa hao.Rais Magufuli
ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu
ya siku ya Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mjini Dodoma.


Pamoja na kutoa
rai hiyo Rais Magufuli ameahidi kuwa atahakikisha azma ya Serikali kuhamia
Dodoma inatekelezwa kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka
mitano.

"Tunapoadhimisha
siku ya Mashujaa hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, Baba wa Taifa alisema makao makuu yawe Dodoma, haiwezekani sisi watoto
wake, sisi wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.


"Kwa hiyo
nilikwishazungumza na leo narudia hili katika siku ya Mashujaa, mlinichagua
ndugu zangu wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi minane
imepita, nimebakiza miaka minne na miezi minne, nataka kuwathibitishia kuwa katika
kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki nitahakikisha serikali yangu
pamoja na mimi tunahamia Dodoma bila kukosa" Amesema
Rais Magufuli.


Kufuatia maelekezo
hayo ya Mhe. Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim
Majaliwa ameagiza Mawaziri wote waanze mara moja kuhamia Dodoma na kwamba yeye
mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.


Viongozi wengine
waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama Janeth
Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia
Ackson, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri Wakuu wastaafu
Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mabalozi na
wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama,
Viongozi wa vyama vya siasa na dini, maafisa na askari waliopigana vita
mbalimbali.


Gerson
Msigwa


Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU


Dodoma