Wanasiasa wakuu nchini Ujerumani wametoa wito kuongezwa kwa masharti magumu kwenye sheria ya udhibiti wa silaha nchini humu, kufuatia kisa cha ufyatuliaji wa risasi uliofanyika mjini Munich siku ya Ijumaa.
Naibu kansela wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, amesema kuwa kila mbinu zitafanywa kupunguza idadi ya raia wanaohitaji kupewa idhini ya kumiliki silaha.

Ali David Son-boly mwenye umri wa miaka 18 aliwauwa watu tisa kwa kuwamiminia risasi na kujiua baadaye huko Munich.
Alikuwa na bastola chapa Glock na zaidi ya risasi 300. Ibada ya ukumbusho kwa wahasiriwa wa waliouwawa itafanyika leo Jumapili mjini Munich.