Watu sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia mabasi mawili eneo la Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Vyombo vya habari nchini humo vinasema watu wawili walifyatulia risasi mabasi hayo yaliyokuwa kwenye msafara.
Watu Zaidi ya 20 wamejeruhiwa.
Mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi anasema shambulio hilo limetokea siku moja tu baada ya Marekani kutoa tahadhari mpya kwa raia wake kuhusu usalama baadhi ya maeneo ya Kenya.
Serikali ya Kenya ilikuwa imetahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulio ya kigaidi huku mfungo wa mwezi wa Ramadhan ukikaribia kumalizika.
Kamati ya usalama katika jimbo la Mandera ilikuwa pia imewaonya watu wasio wa asili ya Kisomali dhidi ya kusafiri eneo hilo kwa kutumia barabara wiki hii.
Shambulio hilo la Ijumaa ndilo la tatu kutekelezwa kwenye mabasi ya uchukuzi wa umma Mandera.


Desemba mwaka jana, watu wawili waliuawa baada ya basi kushambuliwa na watu wenye silaha.
Abiria Waislamu waliwakinga wenzao Wakristo dhidi ya wanamgambo hao waliotaka kuwatenganisha wasafiri hao kwa msingi wa dini.
Novemba 2014 watu wenye silaha waliua abiria 28 walioshindwa kukariri fungu la Koran.
Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa sana na wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabaab kutoka Somalia.
Watu zaidi ya 60 wameuawa katika mashambulio yaliyotekelezwa na kundi hilo eneo hilo katika kipindi cha miaka miwili.