Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniphace Jacob
WATUMISHI wanne wa Idara ya Afya, akiwemo daktari mmoja wa Hospitali ya Sinza Palestina, Alphonce Chiwambo wamefukuzwa kazi baada ya kuthibitika kuwa na makosa ya rushwa na utoro kazini.
Pamoja na kufukuzwa kazi kwa watumishi hao, daktari mwingine wa hospitali hiyo amepewa onyo baada ya kubainika kuwatoza wagonjwa vitu mbalimbali vya matibabu ikiwemo pamba. Watumishi hao wanne waliofukuzwa kazi, ni miongoni mwa watumishi wanane wa Idara ya Afya waliofunguliwa mashauri ya nidhamu.

Katika hatua nyingine, watumishi watatu kati ya tisa wa Idara ya Uhandisi ambao pia walikuwa wakichunguzwa wamethibitika kuwa na hatia na kwa mujibu wa kanuni za utumishi wamepewa adhabu mbalimbali.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniphace Jacob aliyasema hayo jana na kuwataka watumishi wanne waliosimamishwa kuwa ni Athuman Hassan ambaye ni Ofisa Afya wa Mazingira, Martin Malugu (Mteknolojia Msaidizi), Abdulla Ussi (Mteknolojia wa Dawa) na Alphonce Chiwango ambaye ni Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Palestina.
Kwa mujibu wa Jacob, hatua hiyo imekuja baada ya Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo katika mkutano wake maalumu wa mashauri ya nidhamu uliofanyika Julai 26, mwaka huu, pamoja na mambo mengine ulitoa maamuzi kwa watumishi 18 kufunguliwa mashauri hayo.
Alisema mashauri hayo yalikuwa ni dhidi ya watumishi tisa wa Idara ya Uhandisi, watumishi wanane wa Idara ya Afya na mtumishi mmoja wa Idara ya Fedha na Biashara.
Alisema kwa upande wa wahandisi, wawili wameshushwa vyeo na madaraja huku mmoja akishushwa daraja na kupewa onyo na mtumishi mwingine wa Idara ya Fedha na Biashara amepewa onyo kali.
“Uamuzi wa baraza wa kuwapa onyo kali, kuwashusha madaraja na kuwashusha vyeo unatokana na ukweli kuwa walishindwa kutumia taaluma yao vizuri kushauri njia nzuri ya kufanya maamuzi ya mabadiliko ya ujenzi wa barabara za Biafra, Journalism Phase II na Barabara ya Maandazi,” alisema Meya Jacob.
Aliongeza kuwa baraza hilo limezingatia taratibu zote katika kuchukuwa hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi hao, ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa uchunguzi wa awali kuhusu tuhuma na kufungua mashitaka dhidi yao.
Aliagiza watumishi sita waliothibitika kuwa hawana makosa warejee kazini na kuendelea na majukumu mengine. Akielezea sakata la daktari wa Hospitali ya Sinza Palestina, Meya huyo alisema kuwa daktari huyo aliomba rushwa ya Sh 300,000 ili kumfanyia upasuaji mjamzito ambaye alimpatia Sh 250,000 pekee .
Alisema mama huyo alimuahidi Chiwambo kwamba atampatia fedha iliyobaki baada ya kupona, lakini baadaye aliamua kutoa taarifa kuhusu tuhuma hiyo, na kuwezesha daktari huyo kukamatwa.