Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Vuai Ali Vuai
KAMATI ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa, imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa kitulivu na kukitaka kupeleka dukuduku zake zote Septemba 3 na 4 mwaka huu wakati Baraza la Vyama hivyo, litakapokutana kujadili hali ya siasa na amani nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo wakati ikizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo, iliyokutana juzi kupitia taarifa ya maandalizi ya mkutano wa baraza hilo.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Costantine Akitanda alisema ni vyema Chadema na wengine wenye hoja, ajenda na dukuduku zao, wakavuta subira na kuleta hoja hizo katika mkutano huo, ambao ndio mahali pake ili zijadiliwe na kutafutiwa ufumbuzi.
“Ndio maana tunasema subira huvuta heri, haki haitapatikana katika mazingira ya shari, bali majadiliano na kwamba baraza hilo lilianzishwa kwa ajili ya kuleta majadiliano na maridhiano na kwamba Septemba Mosi ni Siku ya Majeshi hivyo hatupendi kuihusisha na masuala ya kisiasa, tusubiri mkutano huo,” alisema Akitanda.
Akitoa taarifa ya kikao cha Kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Vuai Ali Vuai alisema Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo imeafiki kwamba mkutano wa baraza hilo, uliokuwa ufanyike Agosti 29 na 30 mwaka huu ni vyema ukasogezwa mbele ili kutoa nafasi kwa wageni waalikwa ambao sio wajumbe, kupata muda wa kujiandaa na kuhudhuria mkutano huo muhimu kwa mustakabali wa taifa.
“Awali tuliona ni vyema tukaitisha mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini kuzungumza hali ya siasa na amani ilivyo nchini kwa sasa, tumeona mkutano huo ni muhimu kwa taifa na tukaona kuna haja ya kualika wageni wengine ambao sio wajumbe wa mkutano huo, tumeona ni vyema tutoe muda wa kutosha kwao kujiandaa hivyo mkutano tumeusogeza hadi Septemba 3 na 4 mwaka huu,” alisema Vuai.
Alisema wageni walioalikwa kwenye mkutano huo, ambao sio wajumbe ni 29 ambao ni pamoja na viongozi wastaafu, watu maarufu na wenye heshima katika jamii, wanataaluma na wengine ni viongozi wa vyama vya siasa ingawa hakuwataja majina.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi aliwataka Chadema kuwa wavumilivu na kutaka kusubiri mkutano huo ili dukuduku zao zitolewe kwenye mkutano huo na kutafutiwa ufumbuzi.
“Sikupenda kuzungumza nilitaka Kamati ya Baraza la Vyama vya Siasa ndio wazungumzie hili, ila kwa vile naona linatafsiriwa vibaya acha niliweke vizuri, ni kwamba huu mkutano kutokana na umuhimu wake na masuala yote ya siasa kwa sasa nchini, tumeamua kusogeza muda ili watu nje ya wajumbe tuliowaalika wapate muda wa kutosha kujiandaa... ...kwa maana tungesema mkutano ni tarehe 29 na 30 za awali wangesema tumewapa taarifa muda mfupi, yaani geresha ili washindwe kuhudhuria, sasa tumetoa muda wa kutosha na tunaomba wote wenye madukuduku yao wasikimbie waje wayalete ndani ya mkutano huo,” alisisitiza Jaji Mutungi.
Wakati Baraza likisema hayo, Mwenyekiti wa UDP Taifa, John Cheyo ameishauri Chadema kusitisha maandamano yake ya Ukuta, yanayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu, kwa kuwa kuna viashiria vya kuvunja sheria.
Aliwashauri Watanzania kupaza sauti zao na kukataza watoto wao, kuandamana siku hiyo au kwenda kushambulia na kupambana na polisi, badala yake watafute njia nyingine ya kudai haki wanayoitaka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam huku akiwa amefuatana na Kaimu Katibu Mkuu wa UDP, Goodluck ole Medeye, Cheyo alisema Katiba inatoa haki za aina mbalimbali, lakini hakuna dunia yenye haki bila mipaka.
“Katiba tuliyonayo imeweka taasisi ikiwemo Bunge ambalo linatunga sheria ya kukunyang’anya hata wewe haki ya kuishi. Haki ambayo sasa hivi inatutesa ni haki ya kufanya mikutano na maandamano kwa sababu hadi haki ya mikutano ya ndani inakatazwa na hii inatokana na matumizi ya hiyo haki ndiyo yametufikisha hapa,” alisema Cheyo.
“Kutokana na haki hiyo unakuta watu wanaandaa mikutano ya ndani na kutangaza kumshughulikia Rais kwenye mikutano ya hadhara au unaandaa mikutano ya ndani ya kupanga njama za kuvunja sheria na kusababisha uvunjifu wa amani mfano tarehe moja, ni lazima utakatazwa kwa kuwa Rais ndio amepewa mamlaka na ni Amiri Jeshi.”
Alisema mtu akitaka kuutangazia ulimwengu kwamba Rais amevunja Katiba, aende mahakamani na kuwashauri Watanzania kutoandamana Septemba Mosi, kwa kuwa aliyechaguliwa kuwa Rais ni Dk John Magufuli na amefanya mengi yasiyotegemewa katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu na kupinga ufisadi.
“Mimi nawashauri Watanzania mambo mengine lazima tuyakatae, tusikubali watoto wetu kwenda kushambulia na kupambana na polisi, hili halitufai Tanzania, na wote lazima tupaze sauti ya kusema hapana, kwa hili na Chadema wakubaliane na sisi, tafuteni njia nyingine ya kupata hiyo haki mnayozungumza,” alisema.
Nacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Chadema imekubali kutumiwa kama vibaraka kuichafua taswira ya nchi na kwamba wanawalaghai Watanzania kwa kuandaa maandamano yasiyo na kikomo. Kimesema hatua hiyo ni ya uvunjaji wa Katiba ya Nchi, sheria na inalenga kuvunja amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema wanachokifanya Chadema ni kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola na serikali kwa madai kwamba Katiba imewapa uhuru.
Sendeka alisema Katiba haitoi haki na uhuru usio na ukomo na kwamba Ibara ya 29 (5) ya Katiba ya Tanzania, inaelezea kuwa ili mtu afaidi haki na uhuru ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambavyo haitaingilia haki ya watu wengine au maslahi ya umma.
Kwa mujibu wa Sendeka, CCM pia walikuwa wanataka haki hiyo ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa lengo la kunadi chama chao, lakini kutokana na agizo hilo, wametii amri halali ya Rais John Magufuli na Jeshi la Polisi.
Alifafanua kuwa sheria ya vyama vya siasa, imekubali wanasiasa kufanya mikutano kwa lengo la kunadi sera zake na kutafuta wanachama na kwamba ni tofauti na lengo la Chadema ambalo ni kuishtaki serikali kwa wananchi.
“Ninawaomba wananchi muyapuuze maandamano haya na msiunge mkono maandamano yatakayofanyika Septemba Mosi mwaka huu, kwani hiyo sio demokrasia. Wanafifisha jitihada za Rais kwa kutaka kuitangazia dunia kwamba Tanzania sio kisiwa cha amani, wanatafuta umaarufu kupitia migongo ya Watanzania. Hakuna damu itakayomwagika kabla ya yeye anayesababisha fujo kushughulikiwa kikamilifu,’’ alisisitiza.
Habari hii imeandikwa na Ikunda Erick, Hellen Mlacky na Francisca Emmanuel.