Shirika la kimataifa la Save the Children limetahadharisha kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano katika nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Angola kuwa hivi karibuni unaweza kuenea katika nchi za mabara ya ulaya , Amerika na Asia.

Ugonjwa huo unaenezwa na mbu aina ya aedes, wanaopatikana katika nchi nyingi za Afrika Magharibi.
Mlipuko wa ugonjwa huo barani unaelezwa kuwa mkubwa kuliko miaka 30 iliyopita na umesababisha kutumika kwa chanjo mara nne kuliko ilivyo kawaida kwa mwaka huu pekee jambo lililofanya Shrika la Afya duniani WHO kupunguza kiwango cha dozi ili kuwezesha watu wengi zaidi kupata chanjo hiyo.
Shirika hilo la Save the children limesema limetuma wataalamu wake kusaidiana na serikali ya DRC kutoa chanjo homa hiyo ya manjano kwa watu nusu milioni katika mji mkuu wa Kinshasa.
Tayari mzungumko wa kwanza wa chanjo hiyo ilishatolewa katika mji huo wa Kinshasa baada ya kuthibitishwa kulipuka kwa ugonjwa huo ambao hauna tiba.
Awali ugonjwa huo uliripotiwa katika nchi jirani ya Angola kabla ya kuenea nchi Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Zaidi ya watu mia nne walioambukizwa ugonjwa huo wamefariki katika nchi hizo mbili ambapo huku wengine zaidi ya watu elfu sita wakiripotiwa kuambukiza ugonjwa huo.
Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema hakuna maambukizi mapya yaliyoripotiwa nchini Angola tangu mwezi juni , na kufufua matumaini kwamba ugonjwa huo sasa utadhibitiwa.